Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkuu wa upelelezi akana kumhoji Rais Magufuli

11281 Upelelezi+pic TanzaniaWeb

Thu, 12 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kesi imeahirishwa hadi Agosti 7 na 8 mwaka huu

Dar es Salaam. Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala (RCO), Davis Msangi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa hajawahi kumhoji Rais John Magufuli anavyojihisi kutokana na maneno yanayodaiwa kutamkwa na Halima Mdee.

Maneno yanayodaiwa kutamkwa na Mdee Julai 3, 2017 makao makuu ya Chadema yaliyopo Mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni ni “Anaongea hovyohovyo, anatakiwa afungwe breki.”

Inadaiwa mahakamani kuwa maneno hayo yangeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Shahidi huyo alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alipokuwa akihojiwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala kuhusu ushahidi alioutoa mahakamani Juni 29.

Sehemu ya mahojiano kati ya wakili Kibatala na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo:

Kibatala: Unamfahamu huyo John Magufuli na anaishi wapi?

Shahidi: Anaishi Ikulu.

Kibatala: Uliwahi kwenda kumhoji jinsi anavyojisikia kuhusu haya maneno yanayodaiwa kutamkwa na Mdee kwa sababu yeye ndiye mhanga (mhusika)?

Shahidi: Sijawahi.

Kibatala: Uliwahi kuwasiliana na mtu yeyote wa Jeshi la Polisi ili afuate utaratibu kwenda kumhoji?

Shahidi: Hapana.

Kibatala: Unafahamu msimamo wa Bunge kuhusu kauli ya Mheshimiwa Magufuli ya watoto wa kike waliopata mimba wasirudishwe shule?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Tuchukulie mshtakiwa alitamka hayo maneno, unafahamu iwapo alikuwa akirejea kilichosemwa bungeni au la?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Unafahamu chochote kuhusu haki na wajibu wa wabunge?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Unafahamu mshtakiwa ni mbunge?

Shahidi: Nafahamu.

Kibatala: Uliwasiliana na Bunge kama sehemu ya shughuli zako za kiuchunguzi?

Shahidi: Niliwasiliana na Spika kumtaarifu kuhusu kukamatwa kwa Mdee kwa njia ya barua.

Kibatala: Umeitoa mahakamani?

Shahidi: Sijaitoa.

Kibatala: Mdee alikaa kwa muda gani chini ya ulinzi?

Shahidi: Siyo zaidi ya saa 48.

Kibatala: Mshtakiwa anatakiwa apelekwe mahakamani muda gani kwa mujibu wa sheria?

Shahidi: Upelelezi ukikamilika.

Kibatala: Unafahamu Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema nini kuhusu elimu?

Shahidi: Kila mtu ana haki ya kupata elimu kadiri awezavyo.

Kibatala: Kuna mahali inasema mtu akipata ujauzito asirudi shule?

Shahidi: Sifahamu.

Kibatala: Unafahamu Tanzania imetia saini mikataba mbalimbali kuhusu mtoto wa shule kupata elimu?

Shahidi: Sifahamu.

Baada ya mahojiano hayo, Hakimu Simba alisema kesi hiyo imetimiza mwaka mmoja na ilitakiwa hukumu iwe imeshatolewa, hivyo aliuhimiza upande wa mashtaka kupeleka mashahidi.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Patrick Mwita. Kesi imeahirishwa hadi Agosti 7 na 8 mashahidi wa upande wa mashtaka watakapoendelea kutoa ushahidi.

Chanzo: mwananchi.co.tz