Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi wa JATU asomewa masharti ya dhamana

Mkurugenzi Jatu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JATU PLC, Peter Gasaya, akiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Mon, 2 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya JATU PLC, Peter Gasaya( 32) anayekabiliwa na shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh5.1 bilion, ameletwa mahakamani kwa ajili ya kupewa dhamana.

Ni baada ya siku nne kupita tangu alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kwa Mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa Mahakamani hapo Desemba 29, 2022 akikabiliwa na shtaka hilo.

Hata hivyo leo, Januari 2, 2023 wakili wa Serikali Tumaini Maingu ameieleza mahakamani hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya mshtakiwa kupewa dhamana na upande wa mashtaka upo tayari kusikiliza masharti hayo.

Wakili Maingu amedia kifungu 148(5)(e) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya Jinai ( CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2022, kinaruhusu mshtakiwa kupewa dhamana. Hakimu Mrio baada ya kusikiliza maelezo hayo, ametoa masharti matatu dhidi ya mshtakiwa huyo.

Amesema Gasaya anatakiwa kuwasilisha mahakamani hapo fedha taslimu Sh2.6 bilioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo. Pia, mshtakiwa huyo anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotambuliwa kisheria ambao wanabarua kutoka Serikali za Mtaana na wawe na kitambulishi cha Taifa au kitambulisho cha mpiga kura na wawe ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

“Wadhamini hawa wanatakiwa kusaini nusu ya mali iliyotaja kwenye hati ya mashtaka au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani ya Sh 2.6 bilioni na kwamba hati hiyo itabidi ihakikiwe kwanza kabla ya kuletwa mahakamani hapa,” amesema. Hata hivyo, mshtakiwa licha ya kupewa masharti hayo, ameshindwa kutimiza masharti ya hivyo kurudishwa rumande hadi Januari 11, 2023 kesi hiyo itakapotajwa.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 207/2022 yenye shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa anadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh 5,139,865,733 kutoka Saccos ya JATU.

Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya JATU kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataiwekeza kwa kuipanda ili kuzalisha faida zaidi jambo ambalo alijua kuwa sio kweli

Chanzo: Mwananchi