Singida. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Pius Luhende anayedaiwa kuhusika na mauaji ya Isaka Petro (28) amezungumza na Mwananchi akisema “nimepakaziwa tu.”
Luhende alitoa kauli hiyo baada ya mwandishi wetu kumtembelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida alikolazwa tangu Jumanne wiki hii baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.
Kwa mujibu wa mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Ng’hungu Kuzenza, Luhende anasumbuliwa na pumu (asthma) na mapigo ya moyo.
Mkurugenzi huyo ni miongoni mwa watu saba wanaoshikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo yaliyotokea Jumamosi iliyopita katika Kanisa la Wasabato Kijiji cha Kazikazi mkoani humo.
Inaelezwa kuwa mauaji hayo yalitokea baada ya Luhende kuwafuata watuhumiwa wa kosa la kuharibu mali ya mlalamikaji Rose Andrew aliyedai kuharibiwa mali yake iliyopo ndani ya shamba la Tanganyika Packers linalomilikiwa na halmashauri hiyo.
Taarifa ya Polisi inasema kuwa Luhende alipoingia ndani ya kanisa hilo ilitokea vurugu na akaamua kutoka nje kabla ya askari wanyamapori waliokuwa na silaha kufyatua risasi kadhaa na moja ikampiga Isaka na kufariki dunia papo hapo.
Hata hivyo, waumini waliokuwepo katika kanisa hilo wakati mauaji hayo yakitokea walizungumza na Mwananchi na kupingana na polisi wakisema kuwa mkurugenzi huyo ndiye alimfyatulia risasi Isaka.
Luhende ambaye alikuwa akilindwa na askari kanzu wanne wodini alisema bado kifua kinambana mara kwa mara hasa nyakati za usiku.
“Hata hivyo, namshukuru Mungu kwa kunipigania naendelea vizuri kuliko nilipokuwa hospitali ya Manyoni,” alisema Luhende ambaye alikuwa amejilaza kitandani huku mikononi akiwa hajafungwa pingu.
Katika maelezo yake, mkurugenzi huyo alisema amepakaziwa bila kufafanua zaidi kuhusu kauli yake hiyo.
Awali, Dk Kuzenza alisema mkurugenzi huyo alipofikishwa hospitalini hapo alikuwa na hali mbaya akibanwa kifua na tatizo la mapigo ya moyo.
“Tulipompokea alikuwa na hali mbaya kutokana na kubanwa mara kwa mara na kifua. Kwa upande wa mapigo ya moyo tatizo hilo lilianza kupungua. Kwa sasa tatizo la presha tumelidhibiti kiasi cha kutosha,” alisema. Alisema hata tatizo la asthma limeanza kupungua na kwamba atakuwa chini ya uangalizi hadi keshokutwa, “tukijiridhisha kuwa hali yake imeimarika, tutamruhusu kuondoka.”
Wakati huohuo, kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Isaya Mbughi amesema bado wanaendelea kukamilisha hatua za kisheria kabla watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani.
Alisema taratibu hizo zikishakamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. “Luhende endapo atakuwa ameruhusiwa kutoka hospitalini tutamuunganisha,” alisema kamanda huyo.
Juzi, kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike alisema “hatujawapeleka mahakamani, bado kuna taratibu nyingine hazijakamilika, kwa sasa tunaandaa taarifa ya kumpelekea mwendesha mashtaka wa Serikali ambaye ataandaa taratibu za kuwafikisha mahakamani.”
Mgogoro wa ushuru wa mashamba katika mbuga ya Kitongoji cha Boma la kati unatajwa kuwa ndiyo chanzo cha tukio kwani halmashauri inasema mashamba hayo ambayo awali yalikuwa yakimilikiwa na Tanganyika Packers ni sehemu yao.