Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi kampuni ya Jaluma, wenzake kizimbani kwa uhujumu uchumi

93670 Pic+uhujumu Mkurugenzi kampuni ya Jaluma, wenzake kizimbani kwa uhujumu uchumi

Thu, 30 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa kampuni ya Jaluma General Supplies Limited,  Lucas Mallya  na wenzake wanane wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya  kukwepa kodi na kuisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya zaidi ya Sh31.57 bilioni.

Mbali na Mallya washtakiwa wengine ni Emmanuel Peter,  mkurugenzi wa Happy Imports Assosiates, Happy Mwamugunda; Prochesi Shayo; Prokolini  Shayo;  Godfrey Urio;  Nyasulu Nkyapi; Tunsubilege Mateni na Nelson Kahangwa

Akisoma mashtaka hayo leo Jumatano Januari 29, 2020 mbele ya Hakimu mfawidhi, Godfrey Isaya wakili wa Serikali, Faraja Ngukah amedai washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Januari Mosi, 2015 na Januari 7, 2020 maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Nguka amedai mashtaka ya kwanza yanayowakabili ni kuongoza genge la uhalifu.

Amesema Juni 3, 2019 Mallya alitengeneza nyaraka za kodi za kielektroniki ikionesha imetengenezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Inadaiwa Juni 3, 2019  Mallya aliwasilisha hati ya kughushi kuonyesha kuwa stempu za ushuru za  kielektroniki  ni halisi wakati wakijua si kweli.

Pia Soma

Advertisement
Katika shtaka la nne, inadaiwa Januari 7, 2020 maeneo ya Chang'ombe wilayani Temeke, Mallya alikutwa na rola 93 za stempu za ushuru za kielektroniki za Sh80.5 milioni  zilizochapishwa bila mamlaka ya kamishna wa kodi.

Shtaka la tano anadaiwa Januari Mosi, 2016 na Desemba Mosi,  2019 kwa makusudi mshtakiwa huyo alitengeneza stempu za ushuru za kughushi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh15.2 bilioni.

Katika shitaka ya sita anadaiwa kati ya Januari Mosi 2016 na Desemba 31, 2019,   Mallya alitengeneza stempu za kodi za rola 93 na kukwepa kodi ya  Sh15.2 bilioni.

Pia inadaiwa Mallya alijipatia  Sh15.2 bilioni wakati fedha hizo ni mazalia ya makosa ya kukwepa kodi.

Wakili wa Serikali, Zacharia Ndaskoi amedai  Januari 3, 2020  maeneo ya Mbezi Makabe, Peter alikutwa na rola nne za stempu za ushuru za  Sh1,104,000 zilizochapishwa bila kibali cha kamishna wa kodi.

Shtaka la tisa linalomkabili Mwamugunda anadaiwa Januari 3, 2020 bila kusajiliwa na kamishna aliingiza katoni 413 za bidhaa inayoitwa Drostay Hof Wine  ya Sh24,780,000.

Mwamugunda anadaiwa kukwepa kodi ya Sh9.5 bilioni baada ya kuingiza katoni hizo za bidhaa za vilevi, pia anadaiwa kuisababishia Serikali hasara hiyo kwa kushindwa kulipa kodi pamoja na kutakatisha fedha.

Katika shtaka la 12, Proches na Prokolini wanadaiwa kuwa Desemba 19, 2019  walisambaza bidhaa zilizowekwa  stempu za kughushi ambazo ni katoni 749 za Robertson Wine 75CL za Sh 98,670,000;  Drostdy Hof 37.5CL katoni 594 (Sh 12,002,000);  Four Cousins 75 CL katoni 14 (Sh16,240,000) na Amarula 75 CL katoni 58 (Sh 12,120,000). Amesema bidhaa hizo zote ni Sh139 milioni.

Amesema washtakiwa hao wanadaiwa kushindwa  kulipa kodi ya Sh38,827,267 na  Sh2.3 bilioni pamoja na kuisababishia Serikali hasara.

Imedaiwa mahakamani hapo kuwa katika shtaka la 18, Urio akiwa mkurugenzi wa kampuni ya GMU  Group  Limited kati ya Januari Mosi 2015 na Desemba 31,2018 kwa nia ya kukwepa kodi aliwasilisha taarifa za uongo TRA.

Amesema alifanya hivyo na kukwepa kulipa kodi ya Sh4.2 bilioni na kuisababishia hasara Serikali pamoja na kutakatisha fedha.

Mateni na Kahangwa wanadaiwa Januari Mosi 2015 na Desemba 31, 3018 maeneo ya Mbezi Africana walitengeneza taarifa za uongo za mapato za kampuni ya GMU Group Limited kwa mwaka 2015, 2016 na 2017 kwa nia ya kupata faida.

Pia, wanadaiwa walimsaidia Urio kuandaa taarifa za fedha za kampuni hiyo mwaka 2015, 2016 na 2017 kwa lengo la kujipatia faida ya Sh4.2 bilioni wakati wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la kukwepa kodi.

Nkyapi anadaiwa alishindwa kulipa kodi ya Sh89,673,373 na kutoa risiti za kielektroniki baada ya kupokea malipo ya Sh98,670,000 ya Prochesi na Prokolini kwa mauzo ya katoni 759 ya Robertson Wine 75 CL.

Pia, anadaiwa aliingiza bidhaa za vinywaji vikali za Sh95,100,297 bila kusajiliwa na kuisababishia hasara ya Sh89,673,373  kwa kuingiza bidhaa ambazo hazijasajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) pamoja na kutakatisha fedha.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo unaendelea hivyo, waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kukamilisha upelelezi.

Hakimu Isaya aliahirisha kesi hiyo hadi Fabruari 12, 2020 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa kupelekwa rumande kwa sababu mashtaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana kisheria.

Chanzo: mwananchi.co.tz