Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi anayedaiwa kufanya mauaji kanisani kizimbani, arudi gerezani

41388 Pic+itigi Mkurugenzi anayedaiwa kufanya mauaji kanisani kizimbani, arudi gerezani

Wed, 13 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Singida. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Pius Luhende (54) na washtakiwa wengine sita jana walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wakikabiliwa na shtaka moja la mauaji ya Isaka Petro.

Washtakiwa wengine ni Rodney Elias, Makoye Stephen, Erick Paul, Eliutha Augostino, Silivanus Lugwisha na Yusuf John (25).

Mwanasheria wa Serikali, Emil Kiria alidai mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Consolata Singano kuwa Februari 2, eneo la Genge 48 lililopo kijiji cha Kazikazi, Itigi, washitakiwa kwa pamoja walimuua Petro.

Kiria amesema washitakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na sheria kanuni ya adhabu kifungu cha 116 na 197.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Kiria alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ya kutaja kesi hiyo.

Hakimu Singano alisema kwa kuwa kosa hilo halidhaminiki, washitakiwa wataendelea kuwa chini ya ulinzi hadi Februari 25, 2019 itakapotajwa tena.

Baada ya shauri hilo kumalizika, mkurugenzi huyo aliyekuwa amevalia suti ya michezo la rangi ya bluu yenye nakishi za njano, alipanda katika gari jeusi aina ya Toyota Land Cruiser na kupelekwa mahabusu.



Chanzo: mwananchi.co.tz