Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi Temeke mahakamani tena October 19

Lusu Mkurugenzi Temeke mahakamani tena October 19

Fri, 1 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

KESI inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakabibi na Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Edward Haule, imeahirishwa hadi Oktoba 19, mwaka huu.

Kesi hiyo ya matumizi mabaya ya ofisi na madaraka ilitajwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Evodia Kyaruzi.

Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto, alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba shauri liahirishwe hadi tarehe nyingine itakayopangwa.

Mahakama ilikubali kuahirisha hadi Oktoba 19, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wataendelea kuwa nje kwa dhamana.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza, Agosti 20, 2021 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi na shtaka la kwanza ni matumizi mabaya ya ofisi, wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 2020 na Machi 2021 katika Manispaa ya Temeke.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, Mwakabibi akiwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke na Haule akiwa Mratibu wa Mradi wa DMDP, wakiwa waajiriwa wa manispaa hiyo, katika utekelezaji wa ardhi walielekeza ujenzi wa stendi ya mabasi eneo la Buza, kiwanja ambacho kinamilikiwa na Dayosisi ya Kanisa la Anglikana, bila kuwa na ruhusa.

Shtaka la pili ni matumizi mabaya ya madaraka, linaodai Machi 2020 na Machi 2021 katika eneo hilo, washtakiwa kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya kinyume na kifungu cha 3(1) cha Sheria ya Ardhi na kifungu cha 3,4,5,7 na 11 cha Sheria ya Ardhi ya mwaka 2019.

Chanzo: ippmedia.com