Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi Jiji la Mwanza ashtakiwa Tamisemi madai ya kuuza viwanja

Hukumu Pc Data Mkurugenzi Jiji la Mwanza ashtakiwa Tamisemi madai ya kuuza viwanja

Sat, 14 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima 'amemshtaki' mkurugenzi wa jiji hilo, Selemani Sekiete kwa Wizara ya Tamisemi ambayo ndio mamlaka yake ya nidhamu, akimtuhumu kuhusika na uuzaji wa viwanja viwili vyenye thamani ya Sh1 bilioni.

Wakati barua ya mashtaka ikitua Tamisemi, Malima ameagiza watumishi wanne wa jiji hilo kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi kwa tuhuma za uuzaji wa viwanja hivyo.

Viwanja hivyo namba 194 na 195 vipo mtaa wa Rwegasore jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Ijumaa Januari 13, 2023, Malima amewataja wanaosimamishwa kazi kwa nyadhifa zao kuwa ni mhasibu wa Jiji, mwanasheria, ofisa manunuzi na ofisa mipango.

Watumishi hao wa umma wanadaiwa kuuza viwanja hivyo vilivyopo mtaa wa kibiashara katikati ya jiji kwa thamani ndogo kulinganisha na bei ya soko.

Amesema walishirikiana kuuza viwanja hivyo bila kufuata utaratibu kinyume cha taratibu na maadili ya viongozi huku mkurugenzi wa jiji akidaiwa kukiuka maagizo ya kamati ya ulinzi Wilaya ya Nyamagana na ofisi ya mkuu wa mkoa.

"Kwa mamlaka yangu nimeelekeza ofisi ya katibu tawala Mkoa wa Mwanza iwasimamishe kazi watumishi wanne ambao ni wakuu wa idara kupisha uchunguzi na tunaandika barua ofisi ya Rais (Tamisemi) kwa hatua kuhusu mkurugenzi wa Jiji," amesema Malima.

Mkuu huyo wa mkoa amesema licha ya suala la maamuzi kuachwa mikononi mwa Tamisemi, mamlaka ya mkoa unaona kuwa kiongozi huyo amekosa sifa za kuendelea kusalia mkoani humo.

Ameagiza idara ya ardhi kuangaliwa upya pamoja na watumishi hao wanne kuchunguzwa endapo wamehusika katika tukio hilo.

Maazimio ya kikao cha Ulinzi na Usalama wilaya ya Nyamagana Septemba 28, 2022 ilikataza kurejesha au kufanya uwekezaji wowote wa viwanja vitano kuanzia namba 191 hadi 196 bila kamati hiyo kufahamishwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live