Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi Jatu asubiri kupangiwa tarehe ya vikao

Jatu Picbnn Mkurugenzi Jatu asubiri kupangiwa tarehe ya vikao

Mon, 17 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Upande wa mashtaka katika kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya JATU PLC, Peter Gasaya (33), wamesema wanasubiri kupangiwa tarehe ya vikao kwa ajili ya kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo.

Gasaya anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh5.1bilioni na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Aprili 24, 2023 Gasaya kupitia wakili wake, Nafikile Mwamboma, aliiieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa amemwandika barua ya kukiri na kuomba apunguziwe adhabu, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP).

Kutokana na hali hiyo, Mahakama hiyo ilitoa muda kwa upande wa mashtaka kuanza majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo kwa njia ya majadiliano na DPP.

Hata hivyo, leo Jumatatu Julai 17, 2023 Wakili wa Serikali Eva Kassa, ameieleza Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanasubiri kupangiwa tarehe ya kuanza vikao kwa ajili ya kuanza majadiliano ya kuimaliza kesi.

Wakili Kassa amedai kutokana na hali hiyo, wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Kabate baada ya kusikiliza maeneo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 31, 2023.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1bilioni na kutakatisha kiasi hicho katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.

Chanzo: Mwananchi