Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi Jatu ashindwa kufika mahakamani, kesi yakwama

Jatu Picbnn Mkurugenzi Jatu ashindwa kufika mahakamani, kesi yakwama

Mon, 27 Mar 2023 Chanzo: mwanachidigital

Kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh5.1 bilioni, inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JATU PLC, Peter Gasaya imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kile kilichoelezwa na Serikali kuwa mshtakiwa imeshindikana kufikishwa mahakamani hapo.

Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya JATU kwa madai kuwa fedha hizo anazipanda ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.

Kesi hiyo ya jinai namba 207/2022, ilipangwa leo, Machi 27, 2023 kwa ajili ya Serikali kumsomewa mshtakiwa hoja za awali (PH), baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.

Leo, Machi 27, 2023 Wakili wa Serikali Caroline Matemu, ameieleza Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio, kuwa mshtakiwa ambaye yupo Gereza la Keko imeshindikana kuletwa Mahakama kwa ajili ya kusomewa hoja za awali, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea.

"Mheshimiwa hakimu, kesi hii iliitwa kwa ajili ya upande wa mashtaka kumsomea hoja za awali mshtakiwa, lakini kwa bahati mbaya mshtakiwa hajaletwa mahakamani," amedai Matemu na kuongeza

"Kutokana na hali hiyo, tunaomba Mahakama yako itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea hoja za awali (PH)," amedai Matemu.

Matemu baada ya kueleza hayo, makili wa utetezi Nafikile Mwambona akisaidiana na Kung'e Wabeya, waliomba Mahakama itoe hati ya wito ya kumleta mshtakiwa mahakamani ili asomewa PH na kesi hiyo ianza kusikilizwa ushahidi.

Hakimu Mrio amekubaliana na ombi la upande wa utetezi na kisha kutoa hati ya kumuita mshtakiwa kutoka gerezani kwenda mahakamani (Remove Order) na kisha kuahirisha kesi hiyo hadi April 11, 2023.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Gasaya anadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh 5,139,865,733 kutoka Saccos ya JATU.

Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya JATU kwa kujipambanua kwamba fedha hizo atazipanda kama sehemu ya uwekezaji ili kuzalisha faida zaidi jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.

Chanzo: mwanachidigital