Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu mkurugenzi mkuu wa Benki M Tanzania, Sanjeev Kumar kulipa fidia ya zaidi ya Sh6 bilioni na faini ya Sh2 milioni baada ya kukiri mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
Ametakiwa kulipa fidia hiyo ndani ya miezi 24, hadi sasa ameshalipa Sh690 milioni. Kumar ameachiwa huru akitakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha kulingana na muda uliowekwa huku Sh2 milioni akiilipa mahakamani hapo leo.
Uamuzi huo umetolewa baada ya upande wa mashtaka kumfutia mshtakiwa huyo mashtaka ya uhujumu uchumi na kumsomea mashtaka mawili ya kuisababishia Serikali hasara na alikiri kuyatenda.
Akisoma adhabu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema katika mashtaka hayo mawili mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh1 milioni kwa kila kosa.
Amesema pia mshtakiwa atatakiwa kulipa fidia ya zaidi ya Sh6 bilioni katika kipindi cha miezi 24, kila mwezi akipaswa kulipa Sh22.8 milioni
Hakimu Shaidi amesema hati ya kusafiria ya mshtakiwa huyo itabaki katika ofisi za mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) na safari zake zote zitafutiliwa na ofisi hiyo.
Pia Soma
- Mwili wa Mwanakotide kuagwa kesho Dar, kuzikwa Ijumaa Ruvuma
- VIDEO: Viongozi Chadema wamlilia Mwanakotide
- Magufuli ataka haki uchaguzi Serikali za mitaa
Mshtakiwa huyo anadaiwa Januari 20, 2016 akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki M Tanzania kwa vitendo vyake alivyovifanya aliisababishia Serikali kupata hasara ya Sh6 bilioni.
Amesema katika shtaka la pili, mshtakiwa huyo anadaiwa Januari 20, 2016 jijini Dar es Salaam kwa njia ya ulaghai ndani ya Benki M Tanzania akijua ni udanganyifu alijipatia Dola za Marekani 287,000.