Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkulo aomba wakili Magafu asimuulize maswali mengi

66364 WAKILI+PIC

Thu, 11 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa Fedha, Mustafa Mkulo jana alitamani wakili amsamehe kumuuliza maswali, wakati akitoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwenyekiti wa kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya na wenzake wanne.

Mkulo ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa na Wakili Majura Magafu, anayemtetea Kitilya.

Magafu baada ya kumuuliza Mkulo maswali kuhusu ushahidi alioutoa, alisema kuwa kwa kuwa kulingana na maelezo yake yeye (Mkulo) hakuhusika katika mchakato wa mkopo wa Serikali ambao ndio chanzo cha kesi hiyo, basi hata akimuuliza sana atakuwa anamuonea tu.

“Bahati mbaya hukuhusika katika sakata hili, hata nikikuuliza maswali mengine nitakuwa nakuonea maana nitakuwa nakutaka utoe maoni tu,” alisema Magafu huku akitabasamu.

“Nitashukuru sana ukinisamehe,” alijibu Mkulo naye akicheka na baada ya hapo Magafu alikaa chini na kutoa nafasi kwa mawakili wengine wa utetezi kuendelea kumhoji maswali.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya 2019, Shose Sinare na Sioi Solomon, ambao walikuwa maofisa wa Benki ya Stanbic.

Pia Soma

Wengine ni maofisa wa zamani wa Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda na Alfred Misana.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwamo ya kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Dola 6 milioni, kujipatia fedha kiasi hicho kwa udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Immaculata Banzi, Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Katika ushahidi wake, Mkulo alidai kuwa akiwa waziri wa fedha, mwaka wa fedha wa 2011/12 kulikuwa na upungufu katika bajeti wa Dola kama 800 milioni hivyo Serikali ikaanza mchakato wa kutafuta mkopo kufidia upungufu huo.

Alisema katika mchakato huo taasisi mbalimbali za kifedha zikiwamo benki za Stanbic na Standard ziliwasilisha pendekezo kwake kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola 550 na maelezo yote muhimu.

Alisema baada ya kusoma pendekezo hilo, aliandika maelekezo akimwelekeza katibu wake aipeleke kwa kamishna wa sera kwa ajili ya uchambuzi kisha iwasilishwe kwa Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi wa Madeni (TDMC) kuendelea na hatua nyingine zinazofuata.

Alibainisha kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo alikuwa kamishna wa sera ambaye ni mshtakiwa wa nne Shallanda.

Alifafanua kuwa TDMC hufanya uchambuzi wa mapendekezo ya mikopo kisha huwasilisha mapendekezo yake kwa Kamati ya Taifa ya Usimamizi wa Madeni (NDMC).

Aliongeza kuwa NDMC mwenyekiti wake ni Katibu Mkuuwa wizara hiyo na katibu wake ni kamishna wa sera.

Mkulo aliomba mahakama iipokee barua hiyo kama kielelezo ili kitumike kama sehemu ya ushahidi na baada ya mahakama kuipokea barua hiyo alisoma maelezo yaliyomo kuhusiana na mkopo huo.

Baada ya kuisoma Wakili wa Serikali Mwandamizi Pius Hilla aliyekuwa akimuongoza kutoa ushahidi, aliendelea kumuuliza maswali ya kumwongoza kutoa ushahidi.

Alieleza kuwa barua hiyo ilikuwa inapendekeza kuwa Benki ya Stanbic kwa kushirikiana na Benki ya Standard ya Uingereza zingeiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola 550 milioni kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 1.4 ya mkopo huo na kwa riba ya asilimia 6.5

Hata hivyo alisema baadaye aliamua mchakato usitishwe hadi mwaka uliofuata baada ya kushauriwa na wataalamu kwa kuwa mwaka ulikua unaelekea kuisha.

Alisema hata hivyo Mei 2012 aliondoka katika wizara hiyo mchakato huo ukikuwa haujakamilika, lakini mwaka 2016 aliitwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhojiwa kuhusiana na mchakato wa mkopo huo.

Mkulo alisema huko ndiko alipofahamu kuwa baadaye mkopo huo ulitolewa tena Dola 600 milioni na kwa ada ya uwezeshaji wa asilimia 2.4 badala ya asilimia 1.4 ya awali, kiwango ambacho alisema kilikuwa ni kikubwa.

Hata hivyo akiulizwa na maswali na mawakili wengine wa utetezi, akiwemo Jeremiah Mtobesya na Zaharani Sinare wanaomtetea Sinare na wakili Charles Anindo, Mkulo alisema mambo mengine yaliyoendelea nyuma kuhusu mkopo huo hakuyafahamu baada ya kuondoka wizarani hapo.

Chanzo: mwananchi.co.tz