Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkufunzi mbaroni tuhuma rushwa ya ngono

F73c295c82ba03d4b1b0f897f67eb437.jpeg Mkufunzi mbaroni tuhuma rushwa ya ngono

Fri, 9 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) mkoani Kagera, inamshikilia mkufunzi wa Chuo cha Kilimo Maruku kilichopo Halmashauri ya Bukoba mkoani humo, kwa kujihusisha na rushwa ya ngono kinyume cha vifungu vya 15 na 25 vya Sheria ya Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kagera, Joseph John alimtaja mkufunzi huyo kuwa ni Ruta Kyaragaile (59), kutokana na kupokelewa taarifa kutoka kwa mwanafunzi wa kike wa chuo hicho kwa madai amekuwa akisumbuliwa na mwalimu huyo tangu mwaka 2020 akimtaka kushiriki ngono na kutoa vitisho kuwa asiposhiriki hatamaliza masomo.

“Tunamhifadhi jina mwanafunzi na mwaka wa masomo na masomo anayosoma kwa sababu hatua za uchunguzi bado zinaendelea hivyo tunamshikilia mkufunzi huyo kwa sasa,” alisema Kamanda John.

Alisema Takukuru ilianza uchunguzi Aprili 3, mwaka huu ambako maofisa wake walimkamata mkufunzi huyo katika nyumba ya kulala wageni (jina linahifadhiwa) ya Bukoba Mjini akiwa na mwanafunzi huyo akimlazimisha ngono na akitoa baadhi ya vitisho kwa mwanafunzi huyo.

Aidha, alisema uchunguzi upo katika hatua za mwisho na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika na kujibu tuhuma zinazomkabili.

Alisema rushwa ya ngono inatakiwa kupingwa kwani ina madhara makubwa katika jamii na taasisi za umma ambako mtendewa anaweza kupata madhara mbalimbali kama kupata magonjwa, kuathirika kisaikolojia na kupoteza kujiamini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz