Mke wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Hai Lengai Ole Sabaya, ambaye ni shahidi wa utetezi Jesika Thomas (28) amesema atafanya kila kitu isipokuwa kuvunja sheria ili kuhakikisha mume wake anaachiwa huru.
Kadhalika, alikiri mahakamani kwamba laini za simu alizokuwa akizitumia kufanya mawasiliano hazikusajiliwa kwa jina lake bali mume wake alitumia vitambulisho vyake kusajili.
Shahidi huyo, alitoa madai hayo jana mbele ya hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, katika kesi ya uhujumu uchumi.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Othmed Mtenga, shahidi huyo, alikiri kwamba laini ya simu ambayo alikuwa anaitumia hakusajili kwa jina lake bali kwa jina la Sabaya.
Alidai kwamba kwa kuwa hakuwa na Kitambulisho cha Taifa wala namba, Ole Sabaya alitumia kitambulisho chake kumsajilia laini ya simu.
Aliendelea kudai kuwa Januari 22, mwaka 2021, hakujua kama kuna sehemu Sabaya alikwenda mbali na ofisini kwake. Kadhalika akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tersila Gervas, shahidi huyo aliieleza mahakama hiyo, anatambua haki zake ikiwamo haki ya kumiliki mali na kwa jina lake.
Vile vile, alidai katika mali wanazomiliki zipo ambazo zimeandikwa kwa jina lake ikiwamo gari aina ya VX Masai T342 ANT, na nyingine zimeandikwa kwa majina ya Sabaya.
Alidai laini aliyokuwa anatumia kwa ajili ya kufanya mawasiliano ya kibiashara ilisajiliwa mwaka 2018 kwa ajili ya matumizi binafsi.
Pia alidai kwamba sehemu waliyokamatwa huko Mbezi, mkoani Dar es Salaam ilikuwa ni hotelini na sio ‘apartment’. Alidai kwa mujibu wa mila za Kimasai haruhusiwi kushughulika na suala la mifugo. Kwamba fedha zilizokuwa zinapatikana kutokana na mauzo ya mifugo hiyo walikuwa wanaziweka benki.
“Sabaya alikuwa anafanya biashara ya kuuza mbuzi na ng'ombe, lakini kwa mujibu wa mila zao za Kimasai wanawake hawaruhusiwi kujihusisha na mifugo hivyo akishafanya hela analeta nyumbani bila ya mimi kujua alifanya vipi biashara yake," alidai shahidi huyo.
Kadhalika, alidai wanamiliki mashamba eneo la Malula, Mkoa wa Tanga hekari 11.
Alidai kwamba Juni 4, mwaka 2021, wakati akihojiwa na TAKUKURU na kutoa baadhi ya vitu vya Sabaya, alivitoa kama mke wake na sio mchumba.
Alidai kwamba yupo tayari kufanya chochote ili mume wake awe huru bila ya kuvunja sheria.
Shahidi huyo alidai ndoa yake na Sabaya ilifungwa katika Kanisa la Arusha Central Church mwaka 2018 na Askofu aliyefungisha ndoa hiyo ni Dk. Lekundayo. Kabla ya kufunga ndoa ilitangazwa kwa wiki tatu.
Akijitetea jana, Sabaya alidai kwamba Januari 22, mwaka jana, hakwenda Mkoa wa Arusha wala kufika katika karakana ya mfanyabiashara Francis Mroso, iliyoko Mbauda jijini humo.
Kadhalika alidai kwamba siku hiyo, hakutoka katika kituo chake cha kazi wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Akiongozwa na Wakili wa Utetezi, Mosses Mahuna, alidai kwamba ni mwanasiasa na aliteuliwa Julai 29, 2018 na alidumu kwa nafasi ya ukuu wa wilaya kwa miezi 32.
Alidai kwamba Januari 22 mwaka 2021, majira ya asubuhi alimuaga mke wake, Jesca Thomas, kwamba anakwenda ofisini kutekeleza majukumu yake na siku hiyo alikuwa na kazi ya kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji na alikaa ofisini hadi majira ya saa 11 jioni.
Alidai kazi ya kutatua mgogoro huo, alikuwa akishirikiana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Hai, Upendo Uwela.
Shahidi huyo alidai kwamba alifunga ndoa na mke wake, Mei 27, mwaka 2018, katika Kanisa la Wasabato Arusha. Pia alidai ili gari la serikali litoke nje ya wilaya lazima dereva apewe kibali na Katibu Tawala wa Wilaya kwa kuwa ndiyo mhusika anayetakiwa kuidhinisha na kutoa posho na mafuta ya safari.
Vile vile, alidai utaratibu wa kutoka ndani ya wilaya moja kwenda nyingine, lazima kutoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa kwa kuwa ndiye kiongozi mkuu.
Alidai kwamba kilichozungumzwa mahakamani na aliyekuwa Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Renatus Msangira, kwamba hakupokea taarifa ya Sabaya, dereva na gari kutoka Wilaya ya Hai ni za ukweli kwa kuwa hakuweza kutoa taarifa kwa kiongozi huyo kwa kuwa hakutoka kituo chake cha kazi Januari 22, mwaka 2021.