Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkenya kortini Moshi akidaiwa kupora Sh5.3 bilioni mwaka 2004

44325 Pic+mkenya Mkenya kortini Moshi akidaiwa kupora Sh5.3 bilioni mwaka 2004

Fri, 1 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Raia mmoja wa Kenya, anayedaiwa kuongoza kundi la wahalifu 10 kuvamia tawi la Benki ya NBC mjini Moshi mwaka 2004 na kupora Sh5.3 bilioni, amerejeshwa nchini na kushtakiwa.

Vyombo vya dola vya Tanzania na Kenya vimetumia siku 5,475 sawa na miaka 15 kuweza kumnasa na kumrejesha nchini, lakini bado havijafanikiwa kuwanasa watu wengine wanaohusishwa na uhalifu huo, wakiwemo raia watatu wa Uganda.

Ushahidi uliotolewa katika kesi mbili tofauti ambazo zilimalizika kwa raia wa Tanzania na Kenya kufungwa miaka 30 jela, ulimtaja raia huyo wa Kenya, Ingoi kuwa ndiye aliyekuwa kiongozi wa genge lililovamia benki hiyo.

Mtuhumiwa huyo, amefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Moshi, Sophia Masati katika kesi namba 35/2019 ya wizi wa mabilioni ya fedha kwa kutumia silaha.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula imedai, Mei 12,2004, mshitakiwa alivamia benki ya NBC kwa mtutu wa bunduki na kupora Sh5.3 bilioni mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Chavula, anayesaidiana na wakili Akisa Mhando, alidai siku hiyo pia mshitakiwa aliiba dola 610 za Australia, dola 1,422 za Canada, Faranga 5,300 za Uswisi, Euro 16,690 na pauni 1,235 za Kiingereza.

Siku hiyo pia, upande wa mashitaka umedai, mshitakiwa aliiba Krona 2,200 za Norway, Krona 2,140 za Sweden, dola 4,532 za Kimarekani na hundi za kusafiria za thamani ya dola 11,050 za Kimarekani.

Halikadhalika mshitakiwa anadaiwa kuiba Sh126.2 milioni ambazo pamoja na fedha za kigeni zilikuwa mali ya NBC Moshi isipokuwa Sh5.3 bilioni ambazo zilikuwa mali ya BoT.

Katika kesi hiyo, waendesha mashitaka wanadai kabla au wakati wa kuiba fedha hizo, mshitakiwa aliwatisha wafanyakazi na wateja waliokuwamo ndani ya benki hiyo ili kufanikisha wizi huo.

Mshitakiwa huyo alikanusha mashitaka hayo na amerudishwa gereza la Karanga mjini Moshi, kwa kuwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mashitaka ya wizi wa silaha hayana dhamana.

Siku 5,475 za kumrejesha nchini

Mwaka 2004, upande wa Serikali ya Kenya ulifungua maombi kwa niaba ya Tanzania, ukiomba Ingoi na raia mwingine wa nchi hiyo, Wilfred Onyango, warejeshwe Tanzania kujibu tuhuma hizo.

Hata hivyo, Februari 21,2004, Hakimu Mkazi wa Nairobi, Diana Mochache alilikataa ombi hilo akisema haionyeshi kama iwapo wangeletwa Tanzania, kungekuwa na usikilizwaji wa haki wa kesi yao.

Mwanasheria Mkuu alikata rufaa Mahakama Kuu ya Kenya na kufungua rufaa namba 96/2005, akisema hakimu Mochache alijiongoza vibaya kisheria katika kufikia uamuzi huo.

Katika hukumu yake aliyoitoa Septemba 17,2008, Jaji Jackton Ojwang alikubaliana na hoja hizo, akisema hana mashaka kwa kuwa utaratibu wa mahakama za Kenya unafanana na wa Tanzania.

Jaji Ojwang alisema katika hukumu hiyo kuwa hati ya kuwakamata watuhumiwa hao ambao hawakuwepo mahakamani, itaendelea kusimama na wakipatikana warejeshwe Tanzania.

Wakati hukumu hiyo ikisomwa, tayari Onyango, alikuwa amekamatwa Tanzania pamoja na watuhumiwa wengine 11 nao raia wa Kenya, wakati wakitokea Msumbiji.

Tangu kutolewa kwa rufaa na Jaji Ojwang, vyombo vya dola nchini Kenya viliendelea kumsaka Ingoi hadi Januari mwaka huu alipokamatwa na baadaye kurejeshwa Tanzania.

TZ ilivyokwaa kisiki Uganda

Wakati Tanzania ikipitia njia hiyo Kenya, mwaka 2004, Mwanasheria Mkuu wa Uganda aliwasilisha maombi ya kutaka watuhumiwa wawili raia wa nchi hiyo warejeshwe Tanzania.

Katika ushahidi uliotolewa mahakama ya Hakimu Mkazi Kampala, ilidaiwa raia hao, Charles Lumago na Shaban Wayabona, walitoroka nchini Tanzania baada ya tukio la NBC, na raia saba wa Kenya.

Hata hivyo katika hukumu yake aliyoitoa Januari 25,2005, Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Kampala, Margaret Mafabi, alilikataa ombi la kurejeshwa Tanzania, kwa watuhumiwa hao.

Hata hivyo muda mfupi tu baada ya kuachiwa huru, watuhumiwa hao walikamatwa tena kutokana na amri ya mkuu wa polisi wa wakati huo nchini Uganda, Meja Jenerali Katumba Wamala.

Siku hiyo hiyo Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali aliyekuwa akiendesha kesi hiyo, Principal Wagona, aliwasilisha kortini ilani ya kukata rufaa kupinga kuachiwa kwa Waganda hao.

Akitoa hukumu hiyo, hakimu Mafabi alisema mahakama yake isingeweza kuamuru warudishwe Moshi kwa kuionea huruma Tanzania kwa vile imeibiwa fedha nyingi, bali amezingatia ushahidi.

Hakimu Mafabi alisema ushahidi unaonyesha watuhumiwa walipata pasi za kusafiria baada ya tukio hilo, hivyo upande wa mashitaka ulitakiwa kuthibitisha walitumia pasi gani kuingia Tanzania.

Alisema ingawa ushahidi unaonyesha watuhumiwa walikamatwa baada ya kutajwa na mtuhumiwa mwingine raia wa Kenya, Patrick Ayisi Ingoi, hakuna ushahidi kuwa aliwataja kwa majina.



Chanzo: mwananchi.co.tz