Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mke wa bilionea Msuya adai kuteswa wakati wa ukamataji

65ab1de0e27612ba444022d1798d5b65 Mke wa bilionea Msuya adai kuteswa wakati wa ukamataji

Wed, 16 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita amedai aliteswa na askari waliomkamata jijini Arusha na kumsafirisha kumpeleka Dar es Salaam.

Miriam alidai mahakamani jana kuwa, askari walimlazimisha akiri kuhusika na mauaji ya dada wa mumewe, Aneth Msuya aliyeuawa Mei 25, 2016 kwa kukatwa mapanga nyumbani kwake Kibada, Kigamboni.

Alitoa madai hayo wakati akijitetea katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, mbele ya Jaji Edwin Kakolaki katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ya mauaji ya Aneth inayomkabili mahakamani hapo.

Katika kesi hiyo ndogo, Miriam kupitia wakili wake, Omary Msemo anapinga maelezo yake ya onyo yasipokelewe na kutumika kama kielelezo katika kesi hiyo kwa kile alichodai kuwa hakuyatoa na aliteswa kabla ya kusaini maelezo hayo.

Miriam alidai alikamatwa Agosti 5, 2016 mjini Arusha na kupelekwa Kituo cha Polisi Central Arusha kwa tuhuma za upotevu wa mawe matatu ya madini ya Tanzanite kutoka katika mgodi wa Tanzanite One ambayo inadaiwa yalipelekwa kwake na mtu aliyetajwa kwa jina la Claud ambaye ni mfanyakazi wa mgodi huo.

Alidai kulikuwa na mizunguko mingi na askari hao ambao awali walimwambia wanataka awapeleke Tanzanite One lakini badala ya kwenda huko waliishia kuzunguka baadaye wakarudi Central kabla ya kwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake.

Alidai baadaye alishangaa askari hao walipomwambia anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya Aneth huku akizungumza maneno mengine mengi yaliyozidi kumshangaza.

"Askari walianza kupekua chumbani kwangu, tukiwa huko mmoja kati yao alitaka niwape dhahabu alizodai nilikuwa nikimringishia mama mkwe wangu, niliwambia sikuwa namringishia kwani tunaishi mikoa tofauti, nilitoa pochi lenye vito vyangu na kumwaga juu ya meza, walichukua cheni nne za dhahabu na kadi za gari katika droo," alidai Miriam.

Alidai baada ya upekuzi huo, alirejeshwa kituo kikuu cha polisi Arusha na baadaye alipakizwa ndani ya gari akiwa na askari hao ambapo baadaye aliwatambua kwa jina la David, Jumanne na Latifa na wengine watatu ambao hakuwafahamu na safari ilianza kuelekea asipokujua huku wakimhoji sababu ya kumuua Aneth.

Alidai msafara huo uliohusisha magari mawili ya askari aina ya Land Cruiser uliendelea akiwa hajui unapokwenda mpaka walipoona kibao kilichoandikwa Tegeta, ambapo David alimwamuru Latifa amfunge kitambaa usoni naye akafanya hivyo na kutoka hapo hakujua alipelekwa wapi zaidi ya kujua kuwa alipelekwa kituo cha polisi.

Miriam alidai akiwa katika kituo hicho aliteswa kwa kupigwa na kitu kizito kwenye nyayo bila kujua ni kitu gani kwa sababu alifunikwa kitambaa usoni.

Alidai mateso yaliendelea na baadaye akahamishiwa katika kituo kingine kilicho karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere.

Miriam alidai waliendelea kumtesa na kumtisha kwa siku kadhaa hadi Agosti 12, 2016 baada ya kuona anaendelea kukataa David na wenzake walienda katika kituo hicho na kumsainisha nyaraka ya uthibitisho wa maelezo ya onyo bila yeye kujua kilichomo katika maelezo hayo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz