Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mke wa Kisena kuunganishwa na mumewe kesi ya uhujumu uchumi

52734 Pic+kisena

Wed, 17 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Aprili 23 kumuunganisha, Florencia Membe mke wa Robert Kisena katika kesi ya  uhujumu uchumi inayomkabili mumewe na wenzake watatu.

Membe ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Zenon Oil Gas Limited, anakabiliwa na mashtaka saba likiwamo la kuisababishia hasara kampuni ya usafiri wa mabasi yaendayo kasi (Udart) kiasi cha Sh 2.4bilioni.

Membe alifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza Aprili 10 mwaka huu akikabiliwa  na mashtaka hayo.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mkurugenzi wa  Udart, Robert Kisena na wenzake bado haujakamilika kwa sababu wanaendelea kutafuta washtakiwa  wengine katika kesi hiyo.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon alieleza kuwa, kesi hiyo ilikwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake bado haujakamilika.

"Upelelezi bado haujakamilika kwa sababu bado tunaendelea kutafuta washtakiwa wengine na niseme tu tumeshampata mmoja ambaye ni Florencia Membe, hivyo tunaomba tarehe ijayo aunganishwe katika kesi hii ya uhujumu uchumi namba 11/2019 inayomkabili mumewe na wenzake watatu," alieleza Simon.

Hakimu Simba alikubaliana na ombi la  upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 23 itakapotajwa.

Kisena na wenzake watatu wanakabili na mashtaka 19 yakiwamo ya utakatishaji fedha katika kesi ya Uhujumu uchumi namba 11/2019.

Mbali na Robert Kisena, washtakiwa wengine ni Kulwa Kisena, mhasibu wa kampuni hiyo, Charles Selemani na raia wa China, Chen Shi.

Hata hivyo, Kulwa Kisena na Charles Selemani hawakuwapo mahakama leo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni wagonjwa.

Kati ya mashtaka hayo 19 yanayowakabili washtakiwa hao, moja ni kuongoza mtandao wa uhalifu; manne ya kughushi nyaraka; manne ya  kuwasilisha nyaraka za uongo na manne ya utakatishaji fedha zaidi ya Sh2.4 bilioni.

Mashtaka mengine ni kujenga kituo cha mafuta bila kibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na kuuza mafuta mahali pasiporuhusiwa (makao makuu ya kampuni hiyo - Jangwani).

Mashtaka mengine ni  kujipatia pesa kwa njia za udanganyifu zaidi ya Sh1.1 bilioni; kuisababishia Udart hasara ya zaidi Sh2.4 bilioni na wizi wa mafuta yenye thamani ya zaidi ya Sh1.2 bilioni mali ya Udart.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Januari Mosi 2011 na Mei 2018 katika ofisi za kampuni hiyo zilizoko Jangwani wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.



Chanzo: mwananchi.co.tz