Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mke na mume mbaroni kwa kukichinja kichanga

Pingu New Mke na mume mbaroni kwa kukichinja kichanga

Wed, 2 Aug 2023 Chanzo: Nipashe

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikilia mume na mke, wakazi wa Kijiji cha Nayeme, wilayani Rombo kwa tuhuma za kuua kichanga anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi miwili au mitatu kwa kumchinja na kumtenganisha kichwa na kiwiliwili kisha kuzika kichwa na kufcha kiwiliwili katikati ya magodoro.

Akidhibitisha tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, alisema Melania Tarimo (32) ambaye ni mama mzazi wa kichanga hicho, kwa kushirikiana na Priscus Daniel, maarufu Mtivei, aliyekuwa anaishi naye baba wa mtoto huyo, wanadaiwa kufanya unyama huo Mei mwaka huu.

“Wananchi pamoja na uongozi wa kitongoji walimjengea shaka mama huyo baada ya kutomwona mtoto wake mchanga. Walianza kudadisi bila mafanikio kisha wakatoa taarifa katika kituo cha polisi. Tulianza uchunguzi na Julai 6 mwaka huu tuliwatia mbaroni wawili hao ambao ni mume na mke.

Kamanda alisema walifanya uchunguzi na kubaini mtoto huyo alishafariki dunia na kuzikwa bila kushirikisha viongozi wa kijiji, ndugu, majirani wala mmiliki wa eneo alikozikwa. “Uchunguzi wa awali ulionyesha mtoto huyo ni wa kike. Mauaji hayo yanadaiwa kufanyika na baada ya kumuua walizika kichwa katika eneo la nyumba hiyo na kiwiliwili kilikutwa kimefichwa katikati ya magodoro yaliyokuwapo katika chumba walichokuwa wakiishi.

“Nyumba waliyokuwa wakiishi, mmliki wake yuko Arusha na wao waliwekwa hapo kwa ajili ya kufanya kazi. Tumefukua eneo tuliloonyeshwa, tumefukua na kukuta mabaki ya fuvu la kichwa na vipande vya nguo,” alisema.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitakura, Eva Moshi, alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa yeye ni miongoni mwa waliobaini tukio hilo baada ya kusikia minong’ono miongoni mwa wananchi wake kuwa Melania hajaonekana na mtoto kwa muda licha ya kujulikana kujifungua. Alianza kufuatilia ili kupata ukweli huo.

“Niliamua kwenda kuonanana mama huyo na kutaka kupata taarifa zaidi za mtoto, hakuwa na majibu yanayojitosheleza.

Mwanzoni alisema yuko nyumbani.Tulipofika nyumbani anapoishi akasema yuko katika kituo cha watoto yatima cha Ngaleku, nilipomtaka twende kituoni huko alikataa.

“Aliniambia mtoto aliugua ghafla na kumkimbiza hospitalini na kupata matibabu na kurudi nyumbani, jioni alizidiwa na kufariki dunia na kwamba walimzika yeye na mumewe. Alinitia shaka nikaenda kutoa taarifa kituo cha polisi na ndipo uchunguzi wa kina ulipoanza.

“Baada ya polisi kufika, mama huyo alieleza ukweli juu ya tukio hilo na kichwa cha kichanga hicho kilikutwa kimefukiwa ndani ya geti la nyumba ya bosi wake na kiwiliwili kilikutwa kimefunikwa katikati ya godoro,” alidai.

Inadaiwa kuwa baada ya Melania kupata mwanamume mwingine waliyeshirikiana kufanya mauaji, walikuwa wakigombana kuhusu mtoto huyo na kuna wakati walimtupa.

“Mara kadhaa wamekuwa wakirushiana mtoto, mwanamume alikuwa akimwambia si wake ndiyo maana wakaamua kumuua ili wazae mwingine,” alidai kiongozi huyo wa kitongoji.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Deogratius Maruba, alisema mwili wa mtoto huyo ukiwa umeharibika, ulipokewa na kuhifadhiwa katika Kituo cha Afya Karume na walitoa taarifa Kituo cha Polisi Karume kwa hatua zingine za kisheria.

“Julai 8, mwaka huu katika Kituo chetu cha Afya Karume tulipokea mwili wa mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi miwili mpaka mitatu ambao ulikuwa umeharibika,” alisema.

Gaudenisia Shirika (89), mkazi wa Ibukoni, wilayani Rombo, akizungumza na mwandishi kuhusu tukio hilo, alisema:

“Ni la ukatili. Mimi siridhiki nalo na ninaomba hatua za kisheria zichukulie zaidi juu ya vijana ambao wafanya matukio kama haya nchini, vijana waache kurukaruka na ninashauri wabunge watunge sheria endapo mtu atabainikakumpa mimba mtu awe na jukumu la kumuoa, akikaidi jela miaka 30.

“Hii itasaidia watu kupunguza ukatili. Enyi wanawake, mtoto ni mali yako. Ikiwa mwanamume amemkataa, usikubali kuua, pambana, Mungu atakusaidia.

“Wazazi tusimamie malezi ya watoto ili wamrudie Mungu na kuacha matumizi ya dawa za kulevya yanayopelekea kukosa uamuzi sahihi.”

Chanzo: Nipashe