Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mke asimulia mumewe alivyochukuliwa ‘kininja’

64562 MKE+PIC

Thu, 27 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mke wa mfanyabiashara mwenye asili ya Kenya aliyepotea amesimulia jinsi mume wake, Raphael Ongangi alivyopotea huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini kusaidia juhudi za kupatikana kwake.

Veronica Kundya alilieleza Mwananchi jana kwamba watu wenye silaha walivamia gari walilokuwemo yeye na mume wake majira ya saa tatu na nusu usiku wakiwa wanaelekea nyumbani kwao Kinondoni wakitokea kwenye mkutano wa wazazi wa shule anayosoma mtoto wao.

Kwa mujibu wa mama huyo mwenye watoto wawili, watu wenye silaha walilizunguka gari lao katika makutano ya Barabara ya Karume na Msasani maeneo ya Oysterbay karibu na ubalozi wa Uganda jijini Dar es Salaam.

“Waliingia kwenye gari na silaha zao, wakanitaka nikae kiti cha nyuma na kutupeleka mpaka Safari Beach karibu na soko la samaki la Msasani,” anasimulia Veronica huku akisema muda wote wa tukio alikuwa akilia.

Amesema baada ya kufika eneo hilo, watu hao walimuacha yeye (Veronica) huku wakimwambia asubiri maelekezo zaidi na baada ya kama saa moja hivi alipokea simu kutoka kwa mume wake akimweleza kwamba aende nyumbani na asiripoti popote.

“Mimi nikaenda moja kwa moja mpaka nyumbani kuangalia kama kuna mtu yeyote alikwenda tulipoondoka na kuona kwamba hakuna mtu aliyefika, nilikwenda kituo cha polisi Oysterbay kuandikisha taarifa ya tukio hilo,” alisema Veronica.

Pia Soma

Alipoulizwa na Mwananchi jana kama ana taarifa zozote zinazohusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa alisema hazifahamu na kwamba watazifanyia kazi zitakapowafikia.

Veronica akielezea jinsi watu hao walivyokuwa alisema walionekana watulivu na wala hafikiri kama walikuwa ni majambazi.

“Hawakuniumiza wala kunifanya chochote isipokuwa kunielekezea bastola tu mwanzoni lakini baadaye wakaiondosha,” anasimulia Veronica.

Veronica anasema mume wake ni mfanyabiashara wa kawaida tu na wala hajawahi kusikia kama ana mgogoro na mtu yeyote au kujihusisha na masuala ya kisiasa.

Chanzo: mwananchi.co.tz