Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkazi Dar atuhumiwa kumuua mkewe

1944 Jail 660x400 Mkazi Dar atuhumiwa kumuua mkewe

Sat, 20 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKAZI wa Kimara Stop Over jijini Dar es Salaam, Erick Bubelwa, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mke wake wa ndoa kikatili, Mercy Mkambala (30), kisha kumpeleka hospitali.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Edward Bukombe, aliiambia Nipashe jana kuwa tukio hilo lilitokea Jumanne saa 11 alfajiri nyumbani kwao maeneo ya Kimara Stop Over.

Alisema wanamshikilia mume wa marehemu kwa sababu inadaiwa ndiye aliyemshambulia kwa kumpiga na kitu chenye ncha kali kwenye paji la uso na kusababisha kifo chake.

“Ni kweli hilo tukio limetokea Juni 16, mwaka huu huko Kimara na tayari Jeshi la Polisi linamshikilia mume wa marehemu kwa kumshambulia mke wake, yeye ndiyo chanzo cha kifo chake,” Kamanda alisema.

Mmoja wa majirani (hakupenda jina lake litajwe) alisema aliamshwa na mume wa marehemu usiku wa tukio kuomba msaada.

Alisema mume huyo alidai mke wake, amejigonga kwenye meza na kudondoka chini na kupasuka hivyo kuvuja damu nyingi.

“Tulipofika nyumbani kwao, badala ya mume kuingia ndani alirudi eneo la geti, tulipomuhoji mbona anarudi getini badala ya kuingia ndani, alitueleza anakwenda kutafuta usafiri, hivyo hatukuweza kuingia ndani tuliendelea kusimama nje hadi aliporudi na bodaboda.”

Jirani huyo alidai mume wake alimuhoji mtuhumiwa kama usafiri aliokuja nao mgonjwa anaweza kupanda ndipo alipojibiwa hapana.

“Tulikubaliana aende kutafuta gari na aliondoka na baada ya muda lilikuja gari aina ya Allex na ndipo tulipoingia chumbani kwa msaada wa mwongozo wa msaidizi wa ndani.

“Wakati huo ilikuwa giza umeme ulikuwa hakuna, tulipoingia chumbani tulimkuta Mercy akiwa amelala kitandani akitokwa na damu nyingi eneo la kichwani na alikuwa hajavaa nguo hivyo tulimsitiri kwa khanga ndipo wanaume walimbeba hadi kwenye gari.”

Alisema waliondoka watu watatu ambao ni mume wa marehemu, dereva ambaye ni mdogo wa marehemu na jirani kuelekea hospitali ya Bhoch iliyopo Kimara.

Alisema baada ya muda majira ya saa tisa usiku taarifa zilirudi kuwa vipimo vya daktari vimeonyesha Mercy amefariki dunia.

Mdogo wa mtuhumiwa, Anna Kurwa, alisema kuwa alifika nyumbani kwa kaka yake kuwasalimia na wakati tukio likitokea alikuwa ndani.

“Tulipoingia ndani (chumbani) kwa kweli kile kitendo kilichofanyika pale hapana, dada alikuwa na majeraha kwenye paji la uso na alivuja damu sana.

“Mpaka sasa swali ninalojiuliza ilikuaje na mbaya zaidi hatukusikia kelele yoyote kwamba kuna nini ili tutoke tuangalie kuna shida gani, kiukweli yule dada ameumia na ameteseka sana hadi kufikia umauti.”

Mama mdogo wa marehemu, Aglipina Dominic, alisema mama wa marehemu alimpigia simu kumjulisha kuwa, amepokea taarifa kuwa Mercy kapigwa na shoti ya umeme chumbani kwao.

“Alijulishwa kuwa shoti ilitokea chumbani akakimbilia sebuleni na akajigonga kwenye meza na kupasuka kichwa damu zinamtoka nyingi na wakati anakimbizwa hospitali akafariki dunia,” alisimulia.

Alisema baada ya kufika eneo la tukio walikuta mlango umefungwa na askari walikuwa wameshakuja na baadaye jioni ulipofunguliwa, hali ya sebule walibaini siyo kweli kama walivyosimulia ikilinganishwa na hali waliyoikuta chumbani.

“Zile damu tulizozikuta kwenye shuka, mito ni kama kitendo kingetendeka sebuleni haya makochi tungekuta yamedondokewa na damu nyingi, lakini hatukukuta chochote sebuleni. Wanandoa hawa walifunga ndoa miaka miwili iliyopita,” alisema.

Mama mkubwa wa marehemu, Letisia Kantunzia, alisema Mercy aliwahi kumweleza mdogo wake kuwa, endapo atafariki azikwe upande wa wazazi wake na siyo wa mume wake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live