Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkataba wa hisa za wafanyakazi TBL wadaiwa kuhalalisha ubadhirifu

72136 Tbl+pic

Tue, 20 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wafanyakazi wa zamani wa kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wanaoishtaki kampuni hiyo wakiituhumu ubadhirifu wa mabilioni ya pesa za Mfuko wa Hisa za Wafanyakazi wake, wameibua utata wa mkataba wa mfuko huo wakidai wadhamini waliweka masharti ya kuhalalisha ubadhirifu walioufanya.

Kutoka na sababu hiyo pamoja na mambo mengine, wafanyakazi hao wanapinga maombi ya TBL kutaka shauri hilo liondolewe mahakamani na lipelekwe kwenye usuluhishi, wakidai hoja hiyo pamoja na hoja nyingine walizoziainisha haziwezi kuamuriwa na msuluhishi isipokuwa mahakama pekee.

Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam nchini Tanzania na makundi mawili ya wafanyakazi wa zamani wa TBL, dhidi ya TBL na wadhamini wa mfuko huo wa hisa wa wafanyakazi, wakiwatuhumu wadaiwa kwa ubadhirifu wa zaidi ya Sh83 bilioni ziliokuwemo katika mfuko huo.

Wadhamini hao ni Arnold Kilewo, David Kvaisving, David Pieterse na Dk Saidi M. Gugu

Wafanyakazi hao wa zamani wa TBL wanaodai ni miongoni mwa wanufaika wa mfuko huo, wanadai Bodi ya Wakurugenzi wa TBL iliuvunja kinyemela na isivyo halali na kujichotea mabilioni ya pesa yaliyokuwemo na kuwagawia hata watu wengine wasio wanufaika huku wao wakitengwa.

Hivyo wanaiomba mahakama hiyo iamuru nao ni wanufaika wa mazao ya mfuko huo na wanastahili kupata mgawo wa pesa hizo, kwa mujibu wa mkataba wa mfuko huo licha ingawa sasa si wafanyakazi tena wa TBL.

Pia Soma

Kesi ya msingi namba 256/2017 inayosikilizwa na Jaji Joaquine De Melo, ilifunguliwa na kundi la wafanyakazi waliokuwa katika nyadhifa za umeneja, wakiwakilishwa na wenzao watano; Oscar Shelukindo na wenzake wanne.

Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, hisa zilizotengwa kwa ajili ya wafanyakazi hao kwenye mfuko huo zilikuwa ni 5,898,596, sawa na asilimia mbili ya hisa za TBL, ambazo hadi 2017, thamani yake kiwango cha chini ilikuwa Sh83 bilioni.

Kundi lingine ni la waliokuwa wafanyakazi wa kawaida linalowakilishwa na wenzao saba, Daniel  Shalua na wenzake sita  ambalo kupitia maombi namba 96 ya mwaka 2018, wanaomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo ya msingi.

Hata hivyo, TBL ilifungua maombi namba 68/2018 ikiomba kesi hiyo iondolewe mahakamani na ipelekwe kwenye usuluhishi, maombi ambayo yalipingwa na kundi la kina Shalua, kupitia kwa wakili wao Kobasi Odhiambo na baadaye kuungwa mkono na kundi la kina Shelukondo.

Katika hoja zao za maandishi walizoziwasilisha mahakamani hapo, ambazo Mwananchi limeziona jana Jumatatu, Agosti 19, 2019, Shalua na wenzake kupitia kwa wakili wao Odhiambo wanadai utata wa mkabata huo na madai yao mengine ni hoja za kisheria ambazo msuluhishi hana mamlaka ya kuyaamua isipokuwa Mahakama Kuu pekee.

Wanadai wakati wa kuandaa mkataba huo, wadhamini na TBL waliweka vifungu ambavyo vinawapa kinga ya kutokuwajibika kwa hasara waliyoisababisha kwa uzembe au kwa udanganyifu kwa kisingizio cha kufanya kwa nia njema kwamba hawawajibiki kwa makosa hayo.

“Kifungu cha 7.4 cha mkataba huwaruhusu wadhamini kufanya malipo kwa mtu yeyote hata kwa wale ambao hawastahili  na hivyo kusababisha hasara bila kuwajibika kwa namna yoyote ile kwa hasara hiyo mradi tu yamefanywa kwa nia njema” wanadai na kuongeza:

“Hivyo wadhamini walitumia kifungu hicho kufanya malipo ambayo hawakuyatolea maelezo kwa kisingizio cha malipo hayo kufanywa kwa nia njema.”

Hoja nyingine za kupinga usuluhishi ni haki yao kuwa wanufaika, jambo ambalo linapingwa na wadaiwa, wao kutokuhusika kusaini mkataba wa uanzishwaji mfuko huo kiasi cha kutokufungwa na masharti ya kwenda kwenye usuluhishi, wadaiwa kufanya vitendo vya udanganyifu.

Chanzo: mwananchi.co.tz