Dar es Salaam. Mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; Miriam Steven Mrita, ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa hakuhusika na mauaji ya wifi yake kwani hata sababu inayotolewa si ya kweli.
Miriam alitoa maelezo hayo jana katika siku ya nne ya utetezi wake kuhusiana na kesi ya mauaji ya wifi yake Aneth Msuya, inayomkabili yeye na mwenzake Revocatus Everist Muyella maarufu kama Ray.
Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Upande wa mashtaka katika ushahidi wake unadai kuwa Miriam alimuua wifi yake kwa sababu ya ugomvi wa mali (mirathi) ya marehemu mumewe Bilionea Msuya na kwamba yeye Miriam alibadili umiliki wa baadhi ya mali hizo na kujimilikisha yeye.
Bilionea Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.
Ushahidi huo ulitolewa na shahidi wa 22 wa upande wa mashtaka, Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Arusha kwa sasa, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), David Mhanaya aliyekuwa kiongozi wa timu ya wapelelezi wa kesi hiyo.
Lakini katika ushahidi wake jana, akiongozwa na wakili wake, Peter Kibatala, alidai kuwa sababu zilizotolewa na upande wa mashtaka siyo za kweli kwani Miriam ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi alidai kuwa hajawahi kuwa na ugomvi wa mirathi na Aneth kwa kuwa hakusa sehemu ya mali hizo wala hajawahi kujimilikisha mali na kwamba vielelezo vya nyaraka mbalimbali alivyoviwasilisha mahakamani vinathibitisha hivyo.
“Mheshimiwa Jaji ili ugomvi wowote utokee kuna sababu. Sasa mimi natuhumiwa kwa mauaji ya Aneth Msuya, kwamba tulikuwa tuna mgogoro wa mali. Vielelezo nilivyovileta hapa ni kuonesha kwamba Aneth hakuwa sehemu ya mali hizo, hakuwa shareholder (mwanahisa) kwenye nyumba, viwanja na hata magari,” amesema Miriam.
Amedai kuwa yeye ndiye aligawa hizo mali akiwa msimamizi wa mirathi hiyo kwa wanufaika yaani watoto wa marehemu na wazazi wake na kwamba ingawa wifi zake hawakuwa wanufaika lakini aliamua kuwagawia sehemu ya urithi huo kwa upendo, kila mmoja Sh73 milioni akiwemo Aneth.
“Kama kungekuwa na mgogoro ungeoneka hapa mahakamani lakini niligawa na kila mmoja akaridhia. Nilifanya hivyo kwa upendo kwani wao (dada wa marehemu) hawakuwa sehemu ya wanufaika,” amedai Miriam na kuongeza:
“Yeye Aneth amesema hakutegemea kama angepata kitu kama hicho kwa hiyo akasema kuwa anashukru amepata kumbukumbu sehemu ya mirathi ya kaka yake kwani alisema atajengea nyumba kama kumbukumbu,” amesema.
Miriam amesisitiza kuwa Anet alikuwa mtoto wake wa kumlea kwani alimlea angali mdogo mpaka akaolewa na kwenda kwa mume wake na kwamba hakuna mahali popote ambako wamewahi kushtakiana.
“Kama kungekuwa na mgogoro baina yangu na Aneth hata upande wa mashtaka ambao ulikuwa na mpelelezi mkuu SSP Mhanaya wangeuleta hapa ushahidi kwamba huyu anatuhumiwa kumuua Aneth kwa ugomvi huu,” amesema.
Hivyo, alidai kuwa ushahidi wote uliotolewa hapo kuwa alipanga njama za kumuua wifi yake huyo ni wa uwongo.
Hata hivyo, Miriam alieleza kuwa alifunguliwa kesi tatu na wazazi wa marehemu mumewe wakiomba aondolewe katika usimamizi wa mirathi hiyo, ambazo zote zilifunguliwa tayari yeye akiwa mahabusu na kwamba katika kesi hizo zote hakuna mahali waombaji walidai kuwa amejimilikisha mali za marehemu.
Amefafanua kuwa shauri la kwanza lilifunguliwa mwaka 2016 na Elisaria Msuya (baba mkwe wake) na wifi yake Dk Ester Elisaria Msuya dhidi yake wakati mimi akiwa mahabusu, wakiomba aondolewe katika usimamizi kwa madai kuwa alichelewa kupeleka mrejesho mahakamani kwa wakati.
Hata hivyo, alieleza kuwa mahaka ilitupilia mbali shauri hilo ikieleza kuwa yeye bado ni msimamizi halali lakini baadaye akafunguliwa shauri lingine na baba mkwe, Elisaria Msuya na Mama mkwe, Ndeshukurwa Msuya ambalo pia lilitupiliwa mbali.
Shari la tatu alidai kuwa lilifunguliwa mwaka 2019 na mama mkwe wake (Ndeshukurwa) ambalo mahakama katika uamuzi wake ilikubaliana na maombi yake ikamuondoa katika usimamizi wa mirathi hiyo.
Alibainisha kuwa aliondolewa kwa sababu ya kuchelewa kuwasilisha mrejesho wa mgawanyo wa mali na kutokana na kuwa mahabusu jambo ambalo linamfanya ashindwe kutekeleza majukumu yake, hivyo wakateuliwa watoto wake wawili waliokamilisha mirathi kuanzia alipokuwa ameishia na mahakama ikaridhika na mirathi ikafungwa Agosti 2022.
“Katika kesi hizo tatu zote hakukuwa na tuhuma za mimi kujitwalia mali. Kama kweli kulikuwa na tuhuma hizo kwamba najimilikisha mali nauza viwanja hao waliofungua ni watu wazima na kwenye maombi yao wangeyatoa. Kwa hiyo tuhuma zilizotolewa na Mhanaya sijui yeye alizitoa wapi.”
Kesi hiyo itaendelea Jumanne Oktoba 31.