Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mjane wa Bilionea Msuya aondolewa hatia

Msuya Msdf Mjane wa Bilionea Msuya aondolewa hatia

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wazee wa Baraza katika kesi ya mauaji inayomkabili mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; Miriam Steven Mrita na mwenzake Revocatus Everist Muyella maarufu kama Ray, wamewaondolea hatia washtakiwa hao.

Wazee hao wa baraza wamewaondolea hatia washtakiwa hao wakati walipotoa maoni yao leo Jumatatu, Desemba 11, 2023 kuhusiana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka pamoja na utetezi wa washtakiwa na mashahidi wao.

Katika maoni yao wazee hao wa baraza kila mmoja kwa wakati wake, wamesema kuwa kulingana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na utetezi uliotolewa na washtakiwa, wanaona kuwa washtakiwa hawana hatia na kuishauri mahakama iwaachilie huru.

Mzee Iddi Hamisi Humba amsema kuwa amepitia ushahidi wa mashahidi 25 na ushahidi wa upande wa utetezi katika mashahidi watano wa utetezi, amejiridhisha kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka pasina kuacha shaka yoyote.

"Kwamba washtakiwa hawa walioko hapa mahakamani ndio waliomuua Aneth Msuya. Kwa maoni yangu Mheshimiwa Jaji washtakiwa hawana hatia. Hivyo ni maoni yangu kwamba Mahakama hii iwaachilie huru", amesema Mzee wa baraza Humba.

Kwa upande wake mzee wa baraza, Omary Panzi amesema kuwa baada ya kusikiliza pande zote anaunga mkono maoni ya mwenzake kuwa amejiridhisha pasina shaka yoyote kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka pasina shaka yoyote.

"Kwa maana hiyo washtakiwa hawana hatia. Ni maoni yangu Mheshimiwa Jaji kuwa washtakiwa waachiliwe huru", amesema mzee Panzi.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, Miriam na mwenzake na Muyella wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji, wakidaiwa kumuua, Aneth Elisaria Msuya, ambaye alikuwa wifi yake (Miriam).

Aneth ambaye aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, Wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Kesi hiyo imeitwa leo kwa ajili ya wazee hao wa baraza kutoa maoni yao kabla ya hukumu rasmi ya Mahakama.

Alichosema jaji

Kabla ya wazee hao kutoa maoni yao, kwanza Jaji Kakolaki amewaelekeza kile wanachopaswa kufanya, alisisitiza kuwa wanapaswa kutoa maoni yao kwa kuangalia ushahidi wa upande wa mashtaka uliowasilishwa mahakamani.

Jaji Kakolaki amesema kwamba ni kanuni ya kisheria kwamba upande wa mashtaka ndio wenye jukumu la kuthibitisha kosa dhidi ya washtakiwa na kwamba ni kanuni kwamba washtakiwa hawatatiwa hatiani kwa sababu tu utetezi wao ulikuwa ni dhaifu.

Badala yake amesema kuwa hatia dhidi ya washtakiwa hutokana na uzito wa ushahidil uliotolewa na upande wa mashtaka na kwamba jukumu la upande wa utetezi ni kutia mashaka tu katika ushahidi wa upande wa mashtaka.

"Kwa hiyo mtaangalia tu uzito wa ushahidi wa upande wa mashtaka na kuangalia kama upande wa utetezi umeweza kuibua mashaka.Mkiona kuna mashaka basi mashaka hayo yanaweza kuwanufsisha washtakiwa", amesema Jaji Kakolaki na kuongeza kuwa mahakama itanufaika na busara zao.

Baada ya maelekezo hayo , Jaji Kakolaki alianza kwa kurejea ushahidi wa upande wa mashtaka na wa utetezi wa washtakiwa, akisoma muhtasari wa ushahidi wa kila shahidi wa pande zote.

Baada ya kusoma muhtasari huo wa ushahidi, Jaji Kakolaki kwa mara nyingine amewaeleza wazee hao jukumu lao na mambo yatakayowaongoza katika kutoa maoni ya kuishauri Mahakama akitoa ufafanuzi wa aina za ushahidi katika kesi za jinai ikiwemo kesi hiyo na ufafanuzi wa misingi ya kisheria inayowaongoza.

Amesema kuwa katika jinai kuna mambo makuu mawili ya kuangalia kitendo chenyewe ambacho mshtakiwa anakuwa anatuhumiwa kukitenda, kama vile kuiba, kumpiga mtu, kuua na kwamba lazima kiwepo kitendo hicho yaani kithibitike kutendeka.

Jambo la pili Jaji Kakalaki amesema kuwa ni kusudio la mtu kutenda kitendo au kosa hilo na kwamba hayo mambo yote mawili ndiyo yanatengeneza kosa.

Amesema kwa mujibu wa kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (PC) mtu atathibitika kuwa na hatia ya mauaji kama atathibitika kuifanya au kuacha kuifanya kitendo ambacho kitasababisha uhai wa mtu kutoweka.

Ametoa mfano wa kitendo nacho mtu anaweza kuacha kukitenda na kusababisha uhai wa mtu kupotea kuwa ni kama vile kumnyima mtu chakula Kwa muda mrefu

Kuhusu nia ovu Jaji Kakolaki amesema inapatikana katika mazingira ya aina tofauti, ikiwa ni pamoja na dhamira ya kutenda kitendo hicho na ufahamu wa madhara ya kitendo husika.

Jaji Kakolaki amesema kuwa kuwepo kwa nia ovu haijalishi kama kifo kimetokea au hakijatokea.

Amefafanua kuwa dhamira ya nia ovu inaangaliwa kwa aina ya silaha, maeneo ya jeraha mwilini, nguvu iliyotumika kwa kutumia silaha hiyo, maneno na vitendo vya kabla ya kile kitendo, vyote hivyo hujenga nia ovu na kwamba mtu akionekana ana nia ovu basi atatiwa hatiani na kwa kesi kama hii adhabu yake ni kunyongwa.

"Hivyo katika kesi hii mtajibu kama hawa washtakiwa ndio waliomuua Aneth Elisaria Msuya au siyo wenyewe", amesema Jaji Kakolaki na kufafanua zaidi:

"Mtaangalia kama kuna mtu amekufa, kama kifo chake hakukuwa cha kawaida na kama washtakiwa ndio wanaohusika na la tatu ni kama mtaona wanaohusika je kitendo walichokifanya kilikuwa kimeambatana na nia ovu?. Kwa hivyo hayo ndio masuala ambayo mtatakiwa kuyatolea majibu."

Azungumzia ushahidi

Pia Jaji Kakolaki ametoa ufafanuzi wa ushahidi wa shahidi wa 21wa upande wa mashtaka daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu Aneth kujua chanzo cha kifo,Dk Hassan Chande, akisema kuwa ni ushahidi wa kitaalamu ambao hata hivyo si lazima uifunge Mahakama kama itaona kuna sababu.

"Kama mtaridhika na ushahidi katika hoja ya kwanza kama marehemu alikufa kifo cha kawaida hamna haja kwenda kwenye viini vingine. Lakini mkiona alikufa kifo kisicho cha kawaida basi sasa mtakwenda katika viini vingine."

Akizungumzia aina ya ushahidi katika kesi hiyo Jaji Kakolaki amewaeleza wazee hao wa baraza kuwa kesi hiyo imejengwa katika ushahidi wa kimazingira kwani hakuna ushahidi wa moja kwa moja kwa maana shahidi aliyeona kitendo cha mauaji kinatokea.

Mbali na ushahidi huo wa kimazingira pia amesema kuwa kuna , kuna ushahidi wa kukiri na ushahidi wa kitaalamu, huku akifafanua kwa ufupi aina hizo za ushahidi, akibainisha kuwa lengo ni kuwafanya wazee hao wa baraza wapate picha na kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa ushauri wao kwa Mahakama.

Akifafanua ushahidi wa kimazingira amesema kuwa si ushahidi wa moja kwa moja bali unalalia kwenye dhana ambayo inahitaji kuungwa mkono na ushahidi mwingine, ili kuweza kufikia kwenye uamuzi; yaani ni muungano wa ushahidi mbalimbali.

Hivyo amesema kuwa katika ushahidi wa aina hiyo upande wa mashtaka, unapaswa kuwasilisha ushahidi ambao haumfanyi mshtakiwa aonekane kuwa hajafanya.

Jaji Kakolaki amesema kuwa aina nyingine ya ushahidi katika kesi hiyo ni shahidi wa kukiri, ambao amesema unaelezwa katika kifungu cha 2 cha Sheria ya Ushahidi.

Amebainisha kuwa ushahidi huĆ³ unaweza kuwa ni kwa maneno ya mdomo au maandishi au kwa vyote viwili, akifafanua kuwa ushahidi wa maandishi ni maelezo yale onyo ( yanayoandikwa wakati mtuhumiwa akihojiwa Polisi) au ya ungamo, maelezo anayoyatoa mtuhumiwa kwa mlinzi wa amani (yaani hakimu wa Mahakama ya Mwanzo).

"Ni msimamo wa kisheria kuwa ushahidi mzuri ni wa yule anayekiri mwenyewe", amesema Jaji Kakolaki na kufafanua zaidi.

"Katika kesi hii mshtakiwa wa kwanza aliyakana maelezo yake. Mahakama bado inaweza kuytumia kumtia hatiani endapo itajiridhisha kuwa kilichomo si kitu kingine bali ukweli na kama itahitaji ushahidi mwingine wa kuunga mkono basi itautafuta huo pia."

Akizungumzia ushahidi wa kitaalamu Jaji Kakolaki amesema unajumuisha pia ushahidi wa vinasaba ambao unakusudia kufanya utambuzi wa mtu katika haki jinai na hata katika kesi za madai kama vile kugombea au kumkana mtoto.

"Huu ni aina ya ushahidi unaowasilishwa mahakamani kutokana na njia za kisayansi kama uchunguzi wa damu, uchunguzi wa vinasaba, uchunguzi wa silaha na unakubalika kwa sababu pia huisaidia Mahakama kufikia uamuzi wake pale ambapo uko nje ya uelewa wake.

Kutofautiana ushahidi

Amesema kuwa katika mazingira ya kawaida kutofautiana kwa ushahidi kunakuwepo na kwamba wa hilo ni jambo la kawaida, lakini akasema kuwa jambo la kuangalia ni kiwango cha kutofautiana.

Jaji Kakolaki amesema kuwa tofauti hizo zinatokana na na kila mtu anavyoangalia jambo, lakini pia tofauti inaweza kutokana na muda au mazingira mfano mtu aliye katika hofu.

Hivyo amesema kuwa sheria inataka kuangalia kama hizo tofauti zinakwenda kwenye mzizi wa hoja za msingi na kwamba kama haziendi kwenye hoja ya msingi wanaweza kuzichukulia kama ni kasoro za kawaida ambazo hazina madhara.

"Lakini kama zinakwenda kwenye hoja za msingi basi hizo zinaathiri kuaminika kwa ushahidi husika", amesema Jaji Kakolaki.

Amewakumbusha kuwa waliwasikiliza na kuwaangalia mashahidi na kwamba wanaweza kupima mwenendo wao kama shahidi fulani alikuwa anasema ukweli au la.

Hata hivyo Jaji Kakolaki amesema kuwa kutokutiwa hatiani kwa mshtakiwa hakuna maana kwamba huyo mshtakiwa hakutenda kosa bali ni mazingira na aina ya ushahidi uliowasilishwa.

"Lakini pia niwaweke wazi kuwa katika kutoa maoni yenu Mahakama haibanwi na maoni yenu inaweza kutofautiana nayo.", amesema Jaji Kakolaki.

Wajibu wa wazee wa baraza

Wazee wa baraza ni sehemu ya akidi katika kesi za jinai zinazosikilizwa na Mahakama Kuu, kama Mahakama itaona ni muhimu kwa maslahi ya haki: kwa mujibu wa kifungu cha 265 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, marekebisho ya mwaka 2022.

Kwa mujibu wa kifungu hicho wazee hao wa baraza wanapaswa kuwa wawili au zaidi kwa kadri Mahakama itakavyoona inafaa, na jukumu lao ni kumshauri jaji kwa masuala ya kiushahidi yasiyohusiana na utaalamu wa kisheria. Hata hivyo ushauri wao haumfungi Jaji katika uamuzi wake. Lengo ni kuwasaidia kufikia uamuzi wa haki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live