Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mjane awasilisha ushahidi kumiliki magari ya kifahari

Mke Wa Marehemu Bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita Mjane awasilisha ushahidi kumiliki magari ya kifahari

Tue, 5 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya, jana amewasilisha mahakamani ushahidi wa magari ya kifahari aliyowahi kuyamiliki yeye binafsi.

Mjane huyo wa Bilionea Msuya, Miriam Steven Mrita anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya wifi yake, marehemu Aneth Msuya, yeye poja na mwenzake Revocatus Everist Muyella marufu kama Ray, amewasilisha ushahidi huó kupitia kwa Wakili wake Peter Kiibatala.

Ushahidi huó ni hati yenye taarifa za umiliki wa magari magari mbalimbali ya kifahari kutoka Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) ambayo wakili wake huyo ameutumia kumhoji shahidi wa 22 wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo kuhusiana na madai aliyoyatoa mahakamani hapo dhidi yake (Miriam).

Aneth alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.

Yeye Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, na mwili wake ulikutwa ndani ya nyumba yake ukiwa uchi na nguo yake ya ndani ikiwa pembeni ya mwili huo.e

Kesi hiyo namba 103/2018 inayosikilizwa na Jaji Edwin Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inaendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Juma.lililopita, pamoja na mambo mengine shahidi wa 22 alidai kuwa Miriam alihusika katika mauaji ya wifi yake kwa kuwa alikuwa na chuki naye kutokana na mgogoro wa mali alizoziacha marehemu Bilionea Msuya ambazo alikuwa akiziuza na na kwamba alikuwa akiziuza na kubadili umiliki wa magari.

Shahidi huyo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) David Paulo Mhanaya alitoa madai hayo wakati akihojiwa na Wakili Kibatala kuhusiana na ushahidi wake wa msingi alioutoa wakati akiongozwa na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri.

SSP Mhanaya alikuwa kiongozi wa timu ya upelelezi wa mauaji hayo iliyoteuliwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Mkosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani Msuya wakati huo, baada ya kutoridhishwa na jinai upelelezi wa awali ulivyokuwa ukiendelea.

Kwa Sasa SSP Mhanaya ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO)

Alitoa mfano wa gari moja aina ya Toyota Landcruiser kuwa lilikuwa inamilikiwa na marehemu Bilionea Msuya lakini mjane wake huyo alibadili umiliki wake akajimilikisha yeye mwenyewe.

Hata hivyo jana Wakili Kibatala ametumia hati hiyo kumhoji shahidi huyo kuhusiana na madai hayo ya mjane huyo wa Bilionea Msuya kubadili umiliki wa magari hayo.

Kwa mujibu was taarifa zilizomo katika hati hiyo, katika ya magari matano yaliyotajwa humo ni gari moja tu lililo katika umiliki wa marehwmu.Bilionea Msuya mpaka kasa.

Magari mengine yote yako katika umiliki wa mjane Huyo wa Bilionea Msuya, huku ikipnesha kuwa awali yalikuwa yakimilikiwa na watu wengine na mengine umiliki wake ulihamishiwa kwa mshtakiwa huyo wakati Bilionea Msuya angali hai.

Maswali ya dodoso

Ifuatavyo ni sehemu ya tatu ya sehemu ya mahojiano hayo aina yake na Wakili Kibatala pamoja na wakili Nehemia Nkoko anayemtetea mshtakiwa wa pili, Muyella.

Kibatala: Shahidi nyie mna case theory( nadharia) kwamba mshtakiwa wa kwanza alianza kubadili umiliki wa magari. TRA ( Mamlaka ya Mapato Tanzania) waliwaandikia barua Julai 20 2017 kuhusu status ya hayo magari uliwahi kuiona?

Shahidi: Sikuwahi kukutana nayo

Kibatala: Kwa hiyo unaposema huyu mama alianza kubadili umiliki una speculate (kisia) tu?

Shahidi: Si-spaculate naongea kitu halisi

Kibatala: Sasa una kitu gani tangible ( dhahiri) ambacho wewe kama senior officer mpelelezi kuiaminisha Mahakama?

Shahidi: Magari yote yalianza kufanyiwa mabadiliko ya umiliki isipokuwa Suzuki Vitara tu.

Kibatala: Hapa kuna taarifa ya kubadili umiliki wa gari Toyota Landcruiser namba T677BNM.Kwa mujibu wa document hiyo gari hilo lilibadilishwa umiliki Desemba 10, 2013, kutoka kwa Samweli Muze kwenda kwa Miriam Mrita. Unafahamu hivyo kwamba umiliki wa gari hilo ulibadilishwa miaka mitatu kabla ya mauaji haya?

Shahidi: Habari ya mwaka sifahamu

Kibatala: Wewe unafahamu hiyo gari Toyota Landcruiser kwa sasa imesajiliwa kwa jina la nani?

Shahidi: Kwanza usiniite wewe, mimi siyo wewe.

Kibatala: Sijakuita wewe mimi nimekuuliza wewe kama.afisa mpelelezi.

Shahidi: Hapana sitaki uniite wewe.

Kibatala: Mheshimiwa Jaji naomba shahidi afundishwe adabu ya hapa mahakamani

Jaji Kakolaki: Shahidi, hapa hatuna ugomvi unachotakiwa ni kujibu maswali.

Shahidi: Sawa Mheshimiwa Jaji, lakini naomba naye asiniite wewe kama kitu kisicho na maana.

Kibatala: Mimi sikuiti nakuuliza kuwa wewe kama Senior Supretendent (Mrakibu Msaidizi) wa Polisi unafahamu gari hiyo imesajiliwa kwa umiliki wa nani?

Jaji Kakolaki: Kwanza umemuonesha hiyo document?

Baada ya swali hilo la Jaji Kakolaki, Wakili Kibatala alimpelekea shahidi kizimbani hati hiyo ya TRA akamkabidhi kisha akamtaka aisome.

Shahidi huyo aliipitia nyaraka kimya kimya.kwa muda kisha akaanza kujibu swali alilokiwa ameulizwa kuhusiana na umiki wa gari hilo aina ya Toyota Landcruiser

Shahidi: Awali ilikuwa katika umiliki wa Michael Joseph Massawe kuanzia tarehe 15/12/2010.

Gari hiyo ilibadilika tena umiliki tarehe 16/11/2011 kuwa na umiliki wa Samweli Muze wa Arusha na baadaye ilibadilishwa tena tarehe 10/12l/2013 kwenda kwa Miriam Steven Mrita Sakina Arusha na tarehe 15/5/2017 ulibadilika umiliki tena kwenda kwa Donald Safari Ltd wa Ngarenalo Arusha.

Mheshimiwa Jaji kipindi hicho chote kulikuwa na kesi ya mirathi ya mume wa huyu Mama, mtuhumiwa( mshtakiwa) wa kwanza, Miriam Bilionea Erasto Msuya ilikuwa inaendelea. Sasa sikutaka kuzungumzia mambo mengine lakini Wakili kwa kuniuliza swali hili amenikumbusha.

Kibatala: Sawa shahidi suala la mirathi ilikuwa nikuulize baadaye baada ya lunch ( chakula cha mchana) lakini kwa kuwa umelileta nakuuliza Sasa, hiyo mirathi unaifahamu ni namba ngapi ya mwaka gani?

Shahidi: Siifahamu wala haihusiani na kesi hii

Kibatala: Ilikuwa Mahakama gani?

Shahidi: Nimesema ilikuwa Moshi

Kibatala: Moshi Mahakama ipi? ya Mwanzo, Wilaya Mahakama Kuu au Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Unafahamu muombaji alikuwa nani?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Unafahamu kuwa huyu mama mshtakiwa wa kwanza aliteuliwa kuwa msimamizi?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Halafu bado unakuja hapa unazungumzia kesi ya mirathi.

Kibatala: Unafahamu kwamba kuteuliwa msimamizi ili ugawe mali ni lazima hiyo mali ije kwa msimamizi kama personal beneficiary (mnufaika binafsi)?

Shahidi: Nafahamu lakini siyo kuuza.

Kibatala: Unafahamu kwamba wakati huo mwaka 2013 wakati huyo Mama anatransfer (anahamisha umiliki) hiyo gari hata Erasto Msuya alikuwa hai?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Sasa shahidi ukisoma.hiyo document ni wapi hiyo gari iliwahi iumilikwa na Erasto Msuya mpaka umu-accuse (unamshtaki) mteja wangu?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji hakuna mahali ambapo imeandikwa gari hii ilikuwa inamilikiwa na Msuya lakini tunafahamu magari yote yanamilikiwa na wanaume..

Kibatala: Hiyo ni sheria au ni ni maoni yako binafsi maana sisi wengine wake zetu wanamiliki magari ingawa sijajua kabila lako?

Shahidi: Mimi naaongea

Kibatala: Unaongea kutokana na nini, sheria au maoni binafsi?

Shahidi: Kutokana na mazoea

Kibatala: Ahaa kumbe unazungumza mazoea

Haya angalia hapo gari ya Rangerover. Kwa sababu ninyi ndio mlioandika barua TRA kuomba taarifa hizo za umiliki wa magari hayo. Hebu mwambie Mheshimiwa Jaji ilikuwa inamililiwa na.nani?

Shahidi: Ilisajiliwa Mei 14, 2013 ilikuwa inamililiwa na God Mwanga and Famili wa Arusha baadaye ilibadilishwa umiliki Desemba 12, 2013 kwenda kwa Miriam Mrita wa SLP 15824 Sakina Arusha.

Kibatala: Sasa mwambie Jaji ni lini gari hiyo imewahi kumilikiwa au kuwa mali ya marehemu Erasto Msuya?

Shahidi: Haijawahi kumilikiwa na marehemu Erasto Msuya lakini tuliitilia mashaka kwa nini ilikuwa inabadilishwabadilishwa

Kibatala: Kwani ni jinai kubadilisha umiliki?

Shahidi: Kwa nini ilikuwa inabadilishwa badilishwa na ubadikiahwaji ulikuwa unafanywa kwa series (mfuatano), ulipaswa kufanywa kwa utaratibu.

Kibatala: Wewe unamfahamu God Mwanga?

Shahidi: Simfahamu

Kibatala: Angalia item ya tatu gari aina ya Ford Ranger, ilisajiliwa lini kwa jina la nani?

Shahidi: ilisajiliwa Julai 4, 2012 kwa jina la Miriam Mrita ambaye ndiye mmiliki mpaka sasa.

Kibatala: Sasa ni iini iliwahi kumilikiwa na Erasto Msuya?

Shahidi: Haijawahi lakini tuliyakamata kutokana na kubadilishwa kwa tarehe zilizofuatana wakati kuna kesi ya mirathi ikiwa inaendelea.

Kibatala: Shahidi 2012 Msuya alikuwa hajafariki ni kesi ipi ya mirathi unayoizungumzia wakati gari inanunuliwa Msuya mwenyewe yuko hai?

Shahidi: Mimi Sifahamu Mheshimiwa.

Kibatala: Twende item namba nne gari Rangerover Ivok, ilisajiliwa lini na kwa jina gani?

Shahidi: Hii ilisajiliwa kwa mara ya kwanza Machi 2, 2012 kwa jina la Erasto Elisaria Msuya wa Mererani Arusha ambaye ndiye mmiliki mpaka sasa na kwa mujibu wa taarifa za shahidi Getruda ndio ilikuwa inatumiwa na watuhumiwa

Kibatala: Sasa ni lini mteja wangu alibadilisha ukimiki wa magari kama ulivyosema kuwa alibadilisha magari yote isipokuwa Suzuki Vitara na kuuza mali?

Shahidi: Mheshimiwa hii (Ford Ranger) haijawahi kubadilishwa.

Kibatala: Angalia item namba Tano Suzuki Vitara, imewajiliwa na kumilikiwa na marehemu Erasto Msuya?

Shahidi: Ilisajiliwa kwa mara ya kwanza tarehe 26/6/2012 kwa jina la Sanshine Express Ltd wa Dar es Salaa. Tarehe 5/7/2012 lilibadilishwa umiliki kwenda kwa Pendael Joel Mollel wa Sakina White Rose Arusha na tarhe27/11/2015 gari hili lilibadilishwa umiliki tena kwenda kw mtuhumiwa wa kwanza Miriam Steven Mrita.

Kibatala: Je ni sahihi kwamba gari hiyo pia haijawahi kumilikiwa na marehemu Erasto Msuya?

Shahidi: Si sahihi kwa majina lakini mali zote zilikuwa kwenye miliki ya Erasto Msuya lakini yamebadilishwa yote.

Kibatala: Shahidi yaani Ford Ranger inenunuliwa 2012 mpaka leo haijabadilishwa wewe mpelelezi unaongea hayo kweli?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji Wakili pia asiongee kama mtu wa mitaani katika hali ya upelelezi haya magari yamebadilishwa mfululizo namna hii kama hii document ya TRA inavyoonesha yeye hawezi kuwa mpelelezi

Kibatala: Sawa Mimi nauliza maswali tu wenye kuamua ni wengine.Haya twende kwenye land (ardhi), kuna ardhi ipi unayoifahamu ambayo mteja wangu alijimilikisha?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji Sifahamu isipokuwa kuna document ambayo tumeikuta kwa mshtakiwa wa pili yenye heka 109 hivi ambayo hati inamhusu mtuhumiwa wa kwanza na familia yake.

Kibatala: Iko kwa majina ya nani?

Shahidi: Majina Sifahamu

Kibatala: Unafahamu kwamba huyo ni dalali na hiyo ardhi ilikuwa inauzwa?

Shahidi: Sifahamu suala la dalali.

Kibatala: Hufahamu na bado wewe ni mpelelezi mahiri

Shahidi: Usinitukane.

Kibatala: Sikutukani, nakuuliza maana wewe ndio umesema ni mpelelezi mahiri

Kibatala: Unafahamu kwamba ndugu wa Erasto waligawiwa mirathi?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Shshidi unafahamu kuwa pamoja na mshtakiwa kukiri kosa kunatakiwa kuwa na ushahidi mwingine unaojitegemea?

Shahidi: Nafahamu

Kibatala: Unafahamu kuwa marehemu na wifi yake mshtakiwa walikuwa wanatumiana meseji fulanifulan?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Hizo meseji ambazo woote upande wa mashtaka unasema walikuwa wanatumiana na ndio zikamchukiza mshtakiwa wewe umewahi kuziona?

Shahidi: Mimi sikuziona.

Kibatala: Mliwahi kuchunguza eneo hilo (ujumbe wa maneno wa simu)?

Shahidi: Walichunguza wengine kama wapo Watakuja kuzungumza...

Kibatala: Nakuuliza wewe Uliwahi kuziona?

Shahidi: Subiri basi mbona unaongea kama wa Manzese? Usinilazimishe nizungumzie ushahidi wa watu wengine kama wapo watakuja kuzungumza hayo ni ya watu wa Cyber watakuja wenyewe.

Kibatala: Hivi yale mambo ya Getruda ( aliyekuwa Binti wa kazj wa marehemu Aneth) uliyoyazungumza hapa siku nzima ulikuwa ni ushahidi wa nani vile?

Shahidi: Kimya

Kibatala: Siku ile (siku shahidi alipotoka Ushahidi wake wa msingi) nilikusikia unataja vifungu vya sheria hapa. Unakifahamu kifungu cha 33 cha CPA (Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai)?

Shahidi: Labda mpaka nikisome

Kibatala: Anampelekea kitabu cha sheria higo na kumuonesha kifungu hicho

Shahidi: Nimekiona (anasema baada ya kukisoma kimyakimya)

Kibatala: Masharti yake unayajua?

Shahidi: Haya wala si ya lazima

Kibatala: Masherti yake unayajua?

Shahidi: Nayajua na hii shall ( neno la Kiingereza lililotumika katika kifungu hicho kuelekeza kinachopaswa kufanyiwa) unayoikimbilia wala si sharti la lazima.

Kibatala: Unafahamu Kiingereza?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Masharti yake ni kwamba mkimkamata mtuhumiwa bila hati ndani ya saa 24 mtoe taarifa kwa Hakimu, mlifanya hivyo?

Shahidi: Hatukufanya hivyo.

Kibatala: Unafahamu masharti ya kifungu cha 38(3) masharti yake ni kwamba unapokamata mali za mtuhumiwa mnapaswa kumpa risiti?

Shahidi: Nafahamu lakini risiti ni suala.mtambuka kwa hiyo tunasaini search warrant ndio inatumika kama.risiti.

Kibatala: Wapi Jaji akisoma ataona kwamba mteja wangu alipewa risiti?

Shahidi: Ninachoweza kusema ni kwamba nilimpa mbele ya mashahidi huru hiyo nakala ya upekuzi ambayo tunai-term (tunachukulia) kama risiti. Mheshimiwa Jaji huyu Wakili hata akienda wapi hawezi kuona Polisi hiyo risiti.

Kibatala: Wapi Jaji akisoma ataona mteja wangu alipewa hiyo risiti?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji huyu Wakili Msomi anaipotezea Mahakama muda maana mimi nitabaki na msimamo wangu kwamba nilimpa nakala ya upekuzi.

Jaji Kakolaki: Hilo swali kimeshajibiwa, tuendelee.

Kibatala: Shahidi ulisema Getruda alikwambia siku mojawapo mteja wangu (mshtakiwa Miriam) alipkwenda kwa marehemu alikuwa na watu watatu waliokuwa wamevaa soksi usoni unakunbuka ulisema hivyo?

Shahidi: Nakumbuka.

Kibatala: Wale watu watatu unawafahamu

Shahidi: Mheshimiwa Jaji mimi siwafahamu hao watu kwa sababu walishatajwa walivaa soksi ndio maana hata Getruda hakuwafahamu

Kibatala: Ulisema baadaye Getruda alipigiwa simu na mtu anaitwa Neema akimwambia Aneth amekufa na kwamba na yeye anatafutwa unakumbuka?

Shahidi: Ndio nakumbuka

Kibatala: Huyo Neema unamfahamu?

Shahidi: Mimi Simfahamu

Kibatala: Ulo-verify (thibitisha) kupitia simu ya Getruda hiyo taarifa?

Shahidi: Siyo tu nilifahamu maana upelelezi huu ulikuwa mpaka na mawasilianao yalifanyika na Neema alipatikana na alihojjwa huko.

Kibatala: Alihojjwa na nani?

Shahidi: Yeye mwenyewe (aliyemhoji) atakuja atasema

Kibatala: Nanataka kujua huyo askari aliyemhoji majina yake unayajua huyajui?

Shahidi: Siyafahamu

Kibatala: Ulisema mlikamata mikufu ya thamani ya mtuhumiwa wa kwanza, sawa?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Hiyo mikufu iko wapi?

Shahidi: Iko kituo cha Polisi

Kibatala: Kipi?

Shahidi: Chang'ombe

Kibatala: Ni afisa gani anaitunza?

Shahidi: Vielelezo vinatunzwa na watunza vielelezo

Kibatala: Ni afisa gani maana mtoto wake anataka afuatilie. Ni miaka 7 sasa lakini mmeishikilia tu au mmeshagawana?

Shahidi: Usini accuse ,hayo ni maneno ya kihuni, Mheshimiwa Jaji

Kibatala: Ulisema mteja wangu alitoa Sh10 milioni kumpa mtuhumiwa wa pili ( kama malipo ya kutekeza mauaji ya Aneth) ulichunguza alitoa lini na kutoka benki gani?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji hiyo fact (jambo) ilikuwa ni ngumu kuchunguza maana huyu alikuwa mfanyabiashara fedha zinaingia hotelini (hoteli anayoimiki) kala wakati.

Kibatala: Uliwahi kuchunguza hayo mauzo hotelini hapo?

Shahidi: Sikuona umuhimu

Kibatala: ulifanya uchunguzi kama mtuhumiwa wa pili alipewa hizo pesa ?

Shahidi: Sikufanya uchunguzi

Kibatala: Ulisema katika hayo ya ukaguzi wa mshtakiwa wa pili (Muyella) uliandika.majina Revocatus Everist P. Mollel (kwenye hati ya upekuzi), ulolipata kwenye cheti cha kuhitimu mafunzo ya mgambo, cheti hicho ulimpa Jaji ili aweze kulinganisha kama huyu mshtakiwa ndiye?

Shahidi: Sikumpa lakini mtuhumiwa huyu ndiye niliyempekua na nikamkuta na kitabu cha bastola chenye jina lake la Revocatus Everist P. Mollel na bastola aina ya Canic.

Na alisaini nikaondoka naye na ndiye huyu yuko hapa mahakamani na vinasaba vyake vilionekana kwenye vielelezo vilivyokutwa eneo la tukio. Sasa akatae kama siyo yeye na kama siyo mhalifu mzoefu.

Kibatala: Hicho kitabu cha umiliki wa bunduki ulimpa Mheshimiwa Jaji Ili aone kama ni mhalifu mzoefu?

Shahidi: Sijampa lakini kikihitajika wataleta.

Kibatala: Mlifanikiwa kupata simu ya marehemu?

Shahidi: Sijakuelewa mheshimiwa Wakili msomi marehemu nani? Lazima u- specify (uainishe)

Kibatala: Ahaa mlifanikiwa kupata simu ya marehemu Aneth Elisaria Msuya?

Shahidi: Sijafanikiwa kuipata.

Kibatala: Mlifanikiwa kuwasiliana na watu wa service provider (kampuni za huduma za simu za mkononi) kuona kama simu za washtakkwa siku hiyo ilikuwa inasoma (manara) Arusha?

Shahidi: Hilo swali nilishalijibu nikasema hawakutumia simu zao walitumia simu maalumu waliyompa Getruda na wakamwambia akimaliza aiharibu.

Kibatala: Hujaelewa swali langu nimekuuliza kama.mlichunguza iwapo simu za washtakiwa siku hiyo (ya tukio) minara ilikuwa inasema Arusha au Dar.

Shahidi: Hilo linahusiana na watu wa cyber ( uhalifu wa kimtandao) wao ndio watakuja kueleza.

Kibatala: Sasa shahidi nimekusikia ulizungumzia maelezo ambayo ulisema mteja wangu aliyaandika kwa Mlinzi wa Amani,( kwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ilala Pangani ambako mshtakiwa Miriam anadaiwa kuwa alikiri kosa) wewe uliyasoma?

Shahidi: Tulishare ( tulishirikishana)

Kibatala: Wewe binafsi uliyasoma?

Shahidi: Nimesema tulishare

Kibatala: Mheshimiwa Jaji sijui utarekodi nini hapo maana namuuliza kama aliyasoma.

Jaji: Shahidi jibu swali kama ulivyoulizwa kama uliyasoma au la

Shahidi: Mheshimiwa Jaji huwa tuna kawaida ya ku - share kila asubuhi taarifa.

Kibatala: Wakati unatoa ushahidi ukitaja namba za usajili wa magari, Getruda akiwatajia hizo namba?

Shahidi: Getruda hakututajia namba alitaja rangi na feature (mwonekano) za magari tulipomkamata (mshtakiwa wa kwanza)0 ndio tukamkuta hizo namba

Kibatala: huyu Getruda mlifuatilia miamala yake?

Shahidi: hatukufuatilia

Kibatala: Hata kama kulikuwa na Sh100 milioni au ngapi?

Shahidi: Hatukufuatilia na wala hatukuona umuhimu wake.

Kibatala: Unaifahamu exhibit register?

Shahidi: Mimi si mtunza vielele

Kibatala: Kuna mtu amekuuliza kuhusu mtunza vielelezo?

Jaji: Shahidi, amekuuliza kama unaifahamu.

Shahidi: Mheshimiwa Jaji ninaifahamu, lakini mimi si mtunza vielelezo.

Kibatala: Kazi yake ni nini?

Shahidi: Kuweka kumbukumbu za vielelezo vilivyokamatwa

Kibatala: Shahidi mlipofanya upekuzi kwa mshtakiwa wa kwanza nilikuuliza kuhusu mikufu, sasa nakuuliza mlichukua hata nguo, nini uhusika wa hizo huó..

Shahidi: Tulizichukua kwa matumizi ya uplelezi

Kibatala: Hiyo mikufu na hizo nguo mpaka leo unatoa hapa ushahidi hizo nguo na hiyo mikufu mlishaiketa (kuziwasilisha mahakamani kama vielelezo)?

Shahidi: Hatujazileta kwa sababu si relevant (hazihusiani) katia shauri hili.

Kibatala: Mwanzoni ulisema kuhusu kesi ya mirathi, Unafahamu kuhusu uwepo wa kesi ya mirathi namba 66 ya mwaka 2019 Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, ambapo mshtakiwa wa kwanza aliteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi?

Shahidi: Siifahamu

Wakili Nehemia Nkoko: Utakubaliana na.mimi baada ya kazi yoote hii ya upelelezi uliandika maelezo yako?

Shahidi: Ndio niliandika.

Nkoko: Utakubaliana na mimi kwamba yote uliyoyaweka kwenye hii statement ( maelezo ya maandishi) ni yale tu ya muhimu ambayo uliona kwamba mtu akisoma atapata picha halisi suala hili?

Shahidi: Ndio Mheshimiwa.

Nkoko: Shahidi kwa kuwa haya ni maelezo yako umeyakubali unataka Mahakama iyapokee kama kielelezo ili iyatumie katika uamuzi wake?

Shahidi: Hapana

Nkoko: Kwa nini hutaki Mahakama iyapokee na Ione makosa yaliyopo na kuyatumia kuwahukumu waashtakiwa?

Shahidi: Hapana, sitaki Mahakama iyapokee kwa sababu mimi niliyaandika katika upelelezi lakini sio kama wewe unavyotaka kuyatumia.

Nkoko: Kwa hiyo kati ya maelezo yako hayo uliyoyaandika wakati huo na ushahidi wako ulioutoa hapa mahakamani unataka mahaka iamini yapi?

Shahidi: Ushahidi wangu nilioutoa hapa ndio wa kweli kabisa.

Mawakili wa utetezi walihitimisha jana hatua ya maswali ya dodosi dhidi ya shahidi huyo wa 22.

Leo shahidi huyo anahitimisha ushahidi wake kwa mahojiano na mwendesha mashtaka. Wakili Kimweri ambaye atamuuliza maswali ya kumuongoza kusawazisha baadhi ya mambo yaliyoibuliwa na mawakili wa utetezi wakati wa maswali ya dodosi Ili kuyatolea ufafanuzi, kabla ya shahidi mwingine kupanda kizimbani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live