Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mishale ya sumu yawaponza watu saba

46299 Pic+mishale Mishale ya sumu yawaponza watu saba

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbulu. Watu saba wakazi wa Bonde la Yaeda Chini wilayani Mbulu mkoani Manyara, wametiwa mbaroni wakidaiwa kuwatishia watumishi wa umma kuwapiga na mishale ya sumu endapo watawakataza kuchungia mifugo kwenye taasisi za Serikali.

Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga ameagiza watu hao wakamatwe kwa kusababisha walimu wa shule za msingi kuhama shule na kukimbilia kusikojulikana.

Akizungumza kwenye kikao cha wananchi na walimu kwenye Bonde la Yaeda Chini, jana Jumatatu Machi 11, 2019 Mofuga amekemea vikali tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga mishale watumishi wa Serikali wanaowazuia kuchungia mifugo kwenye taasisi za umma.

Amesema watu saba wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano wakidaiwa kuwapiga watumishi wa Serikali waliowazuia kuchungia mifugo maeneo ya shule.

Amesema walimu wa Shule ya Msingi Domanga walikimbia kituo cha kazi baada ya kutishiwa na wananchi kuwa watapigwa mishale ya sumu baada ya kuwakataza kuchungia mifugo shuleni hapo.

Amesema hivi karibuni baadhi ya wananchi wa kijiji cha Endagulda walimpiga ofisa mtendaji wa kijiji hicho mshale wa sumu mgongoni kwa sababu ambazo hazijajulikana.

"Hata hivyo nawapongeza waliompa huduma ya kwanza mtendaji huyo kwa kumnywesha mafuta ya kondoo na mkojo wa punda kisha kumpeleka hospitali ya rufaa ya Haydom kwa matibabu zaidi hadi akapona," amesema Mofuga.

Amesema kila mwananchi wa Bonde la Yaeda Chini awe mlinzi wa watumishi wa Serikali kwani wanafanya kazi kwa manufaa ya jamii inayowazunguka na si vinginevyo hivyo wapewe ushirikiano.

"Hivi kweli mwalimu anamfundisha mtoto wako ili miaka ijayo akusaidie wewe, jamii na Taifa kwa ujumla unaweza kumtishia maisha hadi anakimbia kituo chake ni jambo zuri hilo?" Amehoji Mofuga.

Aliwataka askari polisi kuwachukulia hatua kali wale wote watakaofanya uvunjifu wa amani kwenye Bonde la Yaeda Chini hasa vijiji vya Endagulda na Domanga, kata ya Eshkesh.

Hata hivyo, baadhi ya walimu wa eneo hilo walimshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kujali usalama wao kwani wanafanya kazi kwenye mazingira magumu ikiwemo hofu.



Chanzo: mwananchi.co.tz