Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mirathi ya Bilionea Ulomi yagonganisha mahakama

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mirathi ya aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Jubilate Ulomi, inaigonganisha Mahakama Kuu na Mahakama ya Wilaya ya Moshi, baada ya kila moja kutoa uamuzi wake kwa watu tofauti wanaopingana katika uteuzi wa msimamizi wa mirathi hiyo.

Mvutano huo umeibuka baada ya kumalizika kwa mvutano mwingine wa maziko ya mwili wa bilionea huyo uliokuwa kati ya familia na Zainabu Rashid, anayedai kuwa ni mke halali wa Jubilate.

Jubilate, ambaye alikuwa mchimbaji na mmiliki wa migodi kadhaa ya madini ya Tanzanite Mirerani, alifariki dunia Januari 15, katika Hospitali ya Aga Khan Nairobi nchini Kenya na baadaye mwili wake uliletwa nchini kwa ajili ya maziko mkoani Kilimanjaro.

Maziko yake yalikwama kwa muda baada ya Mahakama ya Wilaya ya Hai kuweka zuio baada ya kupokea maombi yaliyowasilishwa na Zainabu, aliyeomba mwili huo usizikwe hadi ufanyike uchunguzi kujua chanzo cha kifo chake huku pia akiomba haki ya kufanya mazishi.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilitengua zuio na kuruhusu familia kuendelea na taratibu za mazishi, siku 17 tangu kufariki kwake, baada ya kupata ripoti ya uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho.

Lakini baadaye, Werandumi Ulomi, anayedai kupendekezwa na marehemu katika wosia kusimamia mali zake, alifungua shauri Mahakama Kuu akiomba ateuliwe kuwa msimamizi wa mirathi hiyo.

Zainabu naye aliomba na akafanikiwa kupata amri ya zuio dhidi ya wanafamilia wa marehemu kutohamisha au kujihusisha na mali za marehemu hadi msimamizi halali atakapoteuliwa kutoka Mahakama ya Wilaya.

Wakati Mahakama ya Wilaya inatoa zuio hilo, Werandumi kupitia kwa wakili wa familia hiyo, Joseph Ngiloi alifungua maombi mengine madogo Mahakama Kuu na akakubaliwa kuteuliwa kuwa msimamizi wa muda wakati shauri la msingi likisubiri uamuzi.

“Kuna uwezekano wa maumivu yanayoweza kusababishwa hasa kwa watoto ambao huhitaji huduma za matunzo, wafanyakazi wa marehemu ambao wanahitaji kulipwa mishahara kuhudumia familia zao na biashara inayoendelea kama hatateuliwa msimamizi wa muda,” alisema Jaji Patricia Fikirini.

Wakili Ngilo alilieleza Mwananchi jana kuwa uamuzi wa Mahakama ya Wilaya si halali na kwamba wanatarajia kuweka pingamizi kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri la mirathi hiyo kwa kuwa inahusisha mali nyingi.

Hata hivyo, Zainabu na mtoto wa marehemu, Julius Jubilate wamewasilisha pingamizi Mahakama Kuu kupinga uteuzi huo wa muda wa Werandumi kusimamia mali za marehemu.

Shauri hilo la mirathi namba 2 la mwaka 2019 linatarajiwa kutajwa Mei 16.

Jubilate ameacha mali kama magari, nyumba, migodi ya Tanzanite na mashamba. Mali hizo ziko sehemu mbalimbali nchini.



Chanzo: mwananchi.co.tz