Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Milioni 33 za Masista zamfikisha mfanyabiashara kwa pilato

83857 Pic+tapeli Afikishwa kortini kwa tuhuma za kuwatapeli masista Sh33 milioni

Thu, 14 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfanyabiashara, George Mapalala(47) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kutakatisha fedha kiasi cha Sh33 milioni mali ya shirika la masista.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwatapeli masista hao na kisha kujipatia Sh33 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Mapalala ambaye ni mkazi wa Mbezi Luis Dar es Salaam  amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu Novemba 11, 2019 na kusomewa Mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa Serikali, Sada Mohamed, amedai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya Uhujumu uchumi namba 120/2019.

Amedai katika shtaka la kwanza, Mapalala anadaiwa Machi 15, 2019 eneo la Mbezi Luis kwa Yusuphu, kwa nia ovu alijipatia Sh33,175, 000 kutoka  Shirika la Masista la Wamisionary wa Ekaristi takatifu na uingilishaji mpya Arusha.

Inadaiwa kuwa kwa njia ya udanganyifu, mshtakiwa huyo alijipatia fedha hizo kwa madai kuwa anaenda kuanzisha taasisi mpya, wakati akijua kuwa ni uongo.

Katika shtaka la pili, siku na eneo hilo,  mshtakiwa alitakatisha kiasi hicho cha fedha wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yake, Hakimu Shaidi alisema mshtakiwa hatakiwi kusema chochote mahakamani hapo kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kuwa halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Pia, mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalum kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania(DPP).

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo wa naomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Shaidi, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 25, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Chanzo: mwananchi.co.tz