Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mikopo umiza kwa wastaafu janga

1bcb73caa0badb9ed97be88e36ead74b.png Mikopo umiza kwa wastaafu janga

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MIKOPO yenye riba kubwa yenye masharti magumu (mikopo umiza) imetajwa kuwa ni janga linalotafuna watumishi hususani wanaokaribia kustaafu.

Hali hiyo imefanya watu mbalimbali ikiwamo vyama vya wafanyakazi kushauri zichukuliwe hatua za makusudi kukomesha watu na taasisi zinazoendesha mikopo hiyo.

Wakati Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikiendelea kupambana kwa kusaidia waliodhulumiwa kurejeshewa fedha zao, imeshauriwa utafutwe muarobaini wa kudumu kutokana na vitendo hivyo kuendelea huku baadhi ya waathirika wakiumia bila kutoa taarifa.

Ingawa Takukuru haijatoa taarifa ya jumla ya ukubwa wa tatizo, taarifa za taasisi hiyo kwenye mikoa mbalimbali, miongoni mwa mambo yaliyoonekana kuchukua nafasi ni kuhusu walivyoshughulikia urejeshaji wa fedha zitokanazo na mikopo umiza baada ya waliodhulumiwa kuwasilisha malalamiko yao.

Akizungumza na mwandishi wa HabariLEO juu ya mikopo hiyo umiza, Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo alisema kuwa ameagiza wakuu wote wa Takukuru wa mikoa kuhakikisha wanawachukulia hatua stahiki kampuni au watu binafsi wanaoendesha shughuli za mikopo umiza.

Alisema tayari kumekuwa na jitihada zinazochukuliwa na Makamanda wa Takukuru wa mikoa katika kusaka wanaoendesha mikopo umiza na kuhakikisha fedha zinarejeshwa kwa wahusika waliodhulumiwa huku matapeli hao wakichukuliwa hatua.

“Kama ambavyo imekuwa ikitangazwa na wakuu wa Takukuru wa mikoa kuwa wamefanikiwa kurejesha fedha zilizodhulumiwa kwa wastaafu au hata fedha ambazo watu wengine siyo wastaafu zimefanikiwa kurejeshwa, hiyo inatokana na umakini wa wakuu wa Takukuru katika kuwasaidia wananchi wanaodhulumiwa kwa njia za hiyo mikopo umiza," alisema.

Miongoni mwa waliozungumza na gazeti hili, wameeleza visababishi vya watumishi wengi kujiingiza katika mikopo hiyo na ambavyo waendeshaji wake wamekuwa wakichuma fedha zao.

Walimu ni miongoni mwa waathirika wa mikopo umiza hatua ambayo Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif alisema chama kimekuwa kikiwasisitiza walimu kujiunga na benki yao- Benki ya Walimu Tanzania.

Seif alisema chama kinafahamu ambavyo walimu hususani wanaokaribia kustaafu, wanavyotapeliwa na imekuwa ikiwasisitiza kutumia huduma za kibenki za benki hiyo kukopa na kupewa elimu ya biashara.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia Ufundi Stadi, Ushauri, Habari na Utafiti (RAAWU), Kanda ya Mashariki, Mecky Kimoni alisema pia katika sekta binafsi wapo wastaafu wanaoibiwa kwa kurubuniwa na waendeshaji wa mikopo umiza.

Alisema, Raawu imekuwa ikishirikiana na wadau wengine kuendesha mafunzo ya ujasiriamali yanayoendana na elimu ya ukopaji kwa wafanyakazi wanaokaribia kustaafu ili kuwaandaa na ajira binafsi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mikopo ya Maxima Microfinance, Halima Rehani alisema kuwa katika utoaji wa mikopo kampuni za ukopeshaji huzingatia suala zima la dhamana inayowekwa na wanaoomba mikopo husika.

Alisema wapo wakopeshaji wanaowalaghai wastaafu na kisha kuchukua sehemu za mali zao kiujanja kupitia mikopo wanayowapatia jambo alilosema ni kinyume na kanuni za Benki Kuu zinazoongoza sekta hiyo ya ukopeshaji.

Mkurugenzi wa Huduma za Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Kodi (TRA), Richard Kayombo aliliambia gazeti hili kwamba TRA inapopokea taarifa za uwapo wa kampuni ya aina hiyo na kujihakikishia kuwa imesajiliwa kwa kuhakiki namba yake ya kulipia kodi(TIN) haraka huifuatilia na kudai kodi husika.

Fedha zilizorejeshwa

Katika kuhakikisha suala hilo linakoma, Takukuru imesaidia watu mbalimbali waliodhulumiwa kwa kurejesha fedha zao ikiwamo mkoani Dodoma ambayo Sh milioni 176 za mikopo umiza zilirejeshwa mwezi uliopita kwa wastaafu 17.

Taarifa ya Kamanda Takukuru wa Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo ilitaja kampuni Geniva Credit Shop ya wilayani Kondoa inayomilikiwa na Abubakar Kinyuma maarufu kama Abubakar Mapesa, akikopesha wafanyakazi wanaokaribia kustaafu kwa kuwapatia fedha kidogo kisha kuchukua kadi zao za ATM na kwenda kuchukua mafao yao.

Wamiliki wa kampuni za namna hiyo, wakijua kuwa mfanyakazi wa umma anakaribia kustaafu na ana mafao yake, humuingia na kumrubuni kumkopesha kisha wanachukua kadi ya ATM.

Alitoa mfano wa mwalimu aliyekopeshwa Sh 300,000 lakini akalipishwa Sh milioni nne na bado akanyang'anywa nyumba yenye thamani ya Sh milioni 35. Kibwengo alisema kampuni kama hizo zimekuwa zikichukuliwa hatua kali.

Mkoani Manyara, katika taarifa ya utendaji kazi ya Aprili-Juni mwaka jana, Takukuru alitoa mfano wa Mwalimu Mstaafu, Loth Ndaalu ambaye wakati akisubiri mafao, alikopa kutoka kwa wakopeshaji wa mitaani jumla ya Sh milioni 14.

Bila hiari, aliwekewa riba ya asilimia 300 tofauti na asilimia 41 hivyo walaghai walijipatia Sh milioni 42 ambazo Takukuru mkoa wa Manyara ilizirejesha kwa mwalimu.

Vile vile Januari mwaka huu, Takukuru mkoani Shinyanga ilirejesha nyumba ya familia ya marehemu Edward Mpolosi iliyokuwa imepokwa na mfanyabiashara wa mikopo umiza. Alichukua mkopo wa Sh 300,000 lakini alipochelewesha kulipa deni hilo liliongezeka riba hadi kufikia Sh milioni 10.5.

Wengi waliozungumza na gazeti hili, walisema watu wanaokaribia kustaafu ni waathirika wa mikopo umiza kutokana na mafao kuchelewa jambo ambalo hulazimika kuchukua mikopo kuendesha maisha wakati wakisubiri malipo.

Mstaafu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mwaka 2010, Zakia Nuhu alisema sababu ya wastaafu kuingia kwenye mikopo umiza ni kutokana na kutojiandaa kujiajiri tangu wakiwa kazini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz