Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mihadarati yampeleka jela miaka saba

A8850d6c383ac3629ab5a635a2a0fbd8 Mihadarati yampeleka jela miaka saba

Sat, 23 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja imemhukumu Mohamed Ibrahim (30) kwenda jela miaka saba baada ya kutiwa hatiani kwa kupatikana na dawa za kulevya aina ya heroin, maeneo ya Kikwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hakimu Mohd Subeit alimhukumu mshitakiwa huyo akiwa hayupo mahakamani na kusema adhabu hiyo itaanza atakapokamatwa baada ya kukimbia wakati akiwa katika ulinzi wa polisi.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Huda Othman aliieleza mahakama kwamba mtuhumiwa alikamatwa akiwa na dawa jumla ya kete 28 za heroin maeneo ya Kiwengwa Mafarasi Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Othman alidai kesi hiyo ilitajwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Mahonda Oktoba 19, mwaka huu na jumla ya mashahidi 12 walitoa ushahidi wao dhidi ya mtuhumiwa huyo.

Hata hivyo, alidai kesi hiyo ilichelewa kuanza kusikilizwa kwa nyakati tofauti baada ya mshitakiwa kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Akisoma hukumu, Hakimu Subeit alisema ameridhika na pande zote mbili na kumtia hatiani.

Alisema ametoa adhabu hiyo iwe fundisho kwa vijana wengine ambao wamekuwa wakijishughulisha na kufanya biashara ya dawa za kulevya ambayo ni kinyume na sheria.

Chanzo: www.habarileo.co.tz