Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miaka 5 shambulio la Lissu bado maswali kibao

Mikapiic Data Miaka 5 shambulio la Lissu bado maswali kibao

Fri, 9 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Ikiwa ni miaka mitano imepita tangu Tundu Lissu, aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki ashambuliwe kwa risasi na watu wasiojulikana, maswali kibao yameendelea kuibuka, kuhusu wahusika, sababu za tukio hilo na kwanini halijachunguzwa.

Lissu (54) ambaye sasa ni makamu mwenyekiti wa Chadema - Bara, alikutana na makasa huo mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari lake akijiandaa kushuka nyumbani kwake, Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge vilivyokuwa vikiendelea.

Ni tukio la kwanza kutokea nchini kwa mwanasiasa na au mtu yoyote kushambuliwa kwa risasi 38, kati yake 16 zikiingia mwili, akiwa eneo wanaloishi viongozi mbalimbali wa kisiasa na Serikali.

Mara baada ya shambulizi hilo, mwanasiasa huyo mkosoaji mkubwa wa Serikali alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali.

Baadaye usiku wa siku hiyo, Lissu alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi hadi hadi Januari 6, 2018, alipohamishiwa nchini Ubelgiji kuendelea na matibabu.

Wakati huo, Mkuu Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alisema uchunguzi wa suala hilo unaendelea lakini anayesubiliwa ni Lissu mwenyewe kurejea nchini pamoja na dareva wake.

Jana, Lissu, baba wa watoto wawili pacha, alizungumza na gazeti hili kwa simu lakini na pia kupitia ukurasa wake wa Twitter, akiendelea kuhoji kilichomtokea siku hiyo na hali ilivyo kwa sasa.

Katika ukurasa wake, mwanasiasa huyo aliweka picha za matukio mbalimbali yakionesha alivyoshambuliwa, anavyosafirishwa kwenda Nairobi, akionekana hadharani mara ya kwanza akiwa wodini.

Picha zingine akiwa na mke wake, Alicia Magabe na nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na simu kando ya dereva wa Lissu ambaye alikuwa ameshika nguo za Lissu zenye damu, nje ya Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Kisha aliandika, “risasi 16, miaka mitano na operesheni 25 baadaye, bado nimewakomalia na mapambano yanaendelea! Lakini bado maswali ni yaleyale yamebaki, nani alinishambulia, kwa nini, kwa nini Serikali na polisi hawajafanya uchunguzi, kwa nini nilinyimwa haki zangu ikiwemo matibabu, Rais Samia una jibu lolote tafadhali?

Pamoja na maswali ambayo hajayajapa majibu kwa miaka mitano, hata alipozungumza na gazeti hili, aliyarejea akigusia hata sababu za kuendelea kuwa nje ya nchi hadi sasa.

Kauli hizo za Lissu zilishabihiana na alichokieleza Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika katika ukarasa wake wa Twitter: “IGP na DCI ni vyema mkatumia siku ya leo (jana) kutoa maelezo kwa umma ni kwanini hadi sasa waliomshambulia kwa risasi Tundu Lissu hawajakamatwa.

“Na lini mtaridhia wachunguzi wa kimataifa waje nchini ikiwa vyombo vya ndani vimeshindwa kukamilisha uchunguzi kwa wakati.”

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alipoulizwa na gazeti hili kuhusu hoja hizo za Lissu na Mnyika, alisema suala hilo lilishatolewa ufafanuzi na Jeshi la Polisi kipindi cha nyuma, kwamba upepelezi hauwezi kufanyika bila kuwepo aliyeshambuliwa.

Alibainisha hata sheria inaeleza aliyefanyiwa anapaswa kuwepo kwa kuwa kuna maswali ya msingi anapaswa kuulizwa, ambayo yatalisaidia Jeshi la Polisi katika upelelezi wake.

“Kama wewe ni polisi na unatakiwa kufanya uchunguzi, lazima uanze na aliyefanyiwa, ni sawa na mtu kaibiwa halafu hataki kutoa maelezo, sheria inasema tuanze kwa mtu aliyefanyiwa kwanza, vipo vitu atakavyotusaidia,” alisema Misime.

Msemaji huyo wa polisi alisema, “uchunguzi wa kesi yeyote ya jinai unaweza kuendelea pale waliofanya tukio hilo watakapopatikana.

“Watakapopatikana ndipo pia utajulikana nia ilikuwa ni nini. Jeshi la Polisi kama lilivyowahi kusema uchunguzi wa tukio la Tundu Lilsu bado tunaendelea nao kwa kukusanya ushahidi kutoka katika vyanzo mbalimbali.

“Tulishasema pia aje pamoja na dereva wake ili tupate maelezo yao kwani yatatusaidia kusonga mbele katika uchunguzi wetu, lakini hawajafika.

Alichokisema Lissu

Katika mazungumzo yake na gazeti hili kwa simu jana, Lissu alisema suala la uchungizi wa tukio lake anaendelea kuviachia vyombo vya ulinzi na usalama vyenye jukumu hilo.

“Pale niliposhambuliwa kulikuwa na ulinzi wa kutosha hadi wa CCTV camera, polisi wanaweza kuitumia hiyo CCTV camera ambayo wanajua ilipo, hawahitaji hadi mimi niwepo,” alisema Lissu

“Pamoja na gari yangu kuendeleaa kuwa polisi kwa miaka mitano, kwanza sijui itakuwa kwenye hali gani hadi leo, hakuna taarifa yoyote iliyowahi kutolewa, kuhusiana na uchunguzi tukio kama lile tena kwenye ofisi (nyumba) za Serikali, endeleeni kuvihoji vyombo vinavyohusika,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu kurejea kwake nchini, alisema Lissu alisema kinachofanya asirejee si kwamba nchi haiko salama, bali anahitaji maandalizi, ikiwemo fedha kwani anayo familia pamoja na vitu vya kusafirisha kuligana na muda alioshi nchini Ubelgiji.

“Mwaka wa tano kuishi nje si jambo dogo, kufanya maandalizi kunahitaji muda na fedha pia, Rais aliahidi kunilipa fedha za matibabu lakini hazijalipwa,” alisema Lissu.

“Hata kiinua mgongo ambacho nimelipwa, wenzangu niliokuwa nao bungeni baada ya kuzungumza nao, walisema walilipwa miezi 44, lakini mimi nililipwa miezi 22, sawa na Sh79 milioni ambazo nazo zilikatwa na benki nilipokuwa nadiwa na sikupata hata shilingi, hivyo kuna fedha nyingine zaidi ya Sh110 milioni nimekatwa na hazijulikani zilipoenda,” alisema.

Lissu alisema alipokutana na Rais Samia Februari mwaka huu, Brussels, Ubelgiji miongoni mwa mambo waliokubaliana ni pamoja na kulipwa stahiki zake zote ikiwemo gharama za matibabu na kiinua mgongo chote.

Alisema Rais Samia alimweleza aandike barua inayoelezea madai yake.

“Na mimi nilimwandikia barua Rais ambayo bado sijajibiwa mpaka sasa.”

Kuhusu usalama wake, Lissu alisema haofii chochote kwani alipokutana na Rais Samia alimuhakikishia usalama, lakini pia Serikali kupitia Bunge nayo ilishatoa kauli, hivyo hana wasiwasi na suala hilo.

Kauli ya Serikali kuhusu usalama wa Lissu na wengine waliokimbilia nje ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni bungeni jijini Dodoma Juni 7 mwaka huu akisema, nchi kwa sasa ni salama na haina tishio lolote la kiusalama.

“Hakuna sababu yoyote kwa viongozi wa kisiasa waliopo nje waendelee kuwa huko, warejee na kutoa mchango wao kwa Taifa kwa nchi yao kwani hapa ni kwao,” alisema Waziri Masauni.

Kabla ya tamko hilo la Serikali, mapema mwaka huu, Lissu alitaja masharti sita ya kurejea nchini likiwemo la kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kuhusu shambulio lake na kumhakikishia usalama wake.

Mwanasiasa huyo aliyeanzia siasa zake ndani ya NCCR-Mageuzi mwaka 1992 hadi 1996 na kuhamia Chadema, alisema katika mazungumzo yake na Rais Samia nchini Ubelgiji walizungumza masuala kadhaa, baadhi yakihusu haki zake alizonyimwa baada ya kuvuliwa ubunge.

Jambo lingine Lissu alilobainisha ni kuhusu zuio la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, suala la katiba mpya na mfumo wa kidemokrasia ambao utatenda haki hasa kwenye chaguzi.

Tayari Rais Samia ameunda Kikosi Kazi kinachoendelea kusanya na kuchakata maoni ya wananchi kuhusu demokrasia ya vyama vingi.

Chanzo: Mwananchi