Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mholanzi apigwa faini Sh4 mil kwa mirungi

43494 Pic+mholanzi Mholanzi apigwa faini Sh4 mil kwa mirungi

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mwanamke raia wa Uholanzi, Vania Diemers (37) aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kwenda Uholanzi amehukumiwa kulipa faini ya Sh4 milioni.

Vania alikamatwa Januari 6 mwaka jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) akitokea Nairobi Kenya ambapo ilikuwa abadili ndege iliyokuwa impeleke Amsterdam, Uholanzi.

Hata hivyo, alipokanyaga ardhi ya Tanzania na kufanyiwa ukaguzi na maofisa usalama wa uwanja huo wakiwamo polisi alikutwa na begi lililokuwa na uzito wa kilo 29.359 za mirungi akizipeleka Uholanzi.

Mholanzi huyo alishitakiwa chini ya kifungu namba 15(A)(1) na 2 (c) cha sheria namba 5 ya kudhibiti dawa za kulevya kama ilivyorekebishwa na kifungu namba 9 cha sheria hiyo ya 2017.

Kifungu alichoshitakiwa nacho hakitoi mwanya wa kupigwa faini isipokuwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Moshi, Naomi Mwerinde alisema upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha shtaka la kusafirisha dawa za kulevya badala yake alimtia hatiani kwa kutumia kifungu cha 17(1((b) cha kukutwa na dawa za kulevya ambacho kinaongelea kiwango kidogo cha dawa za kulevya.

Sheria hiyo inatafsiri kiwango kidogo dawa aina ya mirungi na bangi ni kisichozidi gramu 50 ambacho ni kwa matumizi binafsi. Hivyo Hakimu Mwerinde alimuona mshitakiwa ana hatia ya kosa hilo dogo na kumtoza faini ya Sh4 milioni.

Wakili wa kujitegemea wa mjini Moshi, Ibrahim Komu ambaye alimtetea raia huyo wa Uholanzi aliliambia gazeti hili jana kuwa mteja wake alifanikiwa kulipa faini hiyo na yuko huru. Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani mara ya kwanza Januari 11, 2018 na kukiri kukutwa na mzigo huo lakini akasema ni wa rafiki yake wa kiume anayeishi Nairobi ambaye alimpa kuwapelekea marafiki zake Uholanzi na hakujua kama ni dawa za kulevya bali maua. Alikanusha shitaka hilo na kusema anachofahamu Uholanzi bangi ni halali lakini kwa vile hajui mirungi ni kitu gani hakujua kama ni dawa za kulevya akidhani ni maua.



Chanzo: mwananchi.co.tz