Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mhasibu wa Bodi ya Maendeleo ya Utalii afikishwa mahakamani

Mhasibu Pic Mhasibu wa Bodi ya Maendeleo ya Utalii afikishwa mahakamani

Thu, 15 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mhasibu wa Bodi ya Maendeleo ya Utalii, Eliyudi Kijalu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka 205 likiwemo la utakatishaji wa fedha wa zaidi ya Sh4 bilioni.

Wakili wa Serikali, Faraja Nguka akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rhoda Ngimilinga alidai mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka 95 ya kugushi, 95 ya matumizi mabaya ya mamlaka, moja la ubadhilifu na 14 ya utakatishaji wa fedha.

Nguka alidai kati ya Julai Mosi, 2016 na Julai 30, 2019 mshtakiwa huyo akiwa katika ofisi za Wizara ya Maliasili iliyopo Temeke, aligushi vocha mbalimbali zenye thamani ya Sh 4,036, 770,339 huku akijua ni kosa la kisheria.

Pia inadaiwa kuwa tarehe hiyo mshtakiwa huyo akiwa kwenye ofisi hizo katika kutekeleza majukumu yake akiwa kama mhasibu wa Bodi ya Maendeleo ya Utalii kwa makusudi alitumia mamlaka yake kwa kutoa hundi mbalimbali.

Nguka alidai hundi hizo ambazo hazijaidhinishwa na Mkurugenzi wa utalii kwa lengo la kujipatia manufaa binafsi, yasiyostahili ya kiasi cha zaidi ya Sh4 bilioni kutoka akaunti ya bodi ya mfuko huo ipo katika benki ya NMB tawi la Morogoro road.

Katika shtaka moja la ubadhilifu mshtakiwa analodaiwa kutenda kati ya Julai Mosi, 2016 na Julai 30, 2019 akiwa katika ofisi za Wizara ya Maliasili iliyopo Temeke, alijinufaisha kiasi cha zaidi ya Sh4 bilioni.

Wakili Nguka alidai mshtakiwa huyo pia anakabiliwa na mashitaka 14 ya utakatishaji fedha ambapo inadaiwa alijipatia mali mbalimbali huku akijua mali hizo ni zao la makosa tangulizi ya kugushi na matumizi mabaya ya madaraka.

Katika shtaka lingine inadaiwa kuwa mshitakiwa huyo katika tarehe hizo wizarani hapo jijini Dar es Salaam,aliisababishia Mfuko wa Maendeleo ya Utalii hasara ya kiasi cha Sh4,036, 770,339.

Nguka alidai upelelezi wa kesi hiyo unaendelwa na kesi iliahirishwa hadi Juni 28,2023 huku mshtakiwa huyo alipelekwa mahabusu kwa kuwa mashtaka ya utakatishaji hayana dhamana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live