Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mhasibu bodi ya pamba aachiwa huru

68068 PIC+HURU

Wed, 24 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  imemuachia huru mhasibu mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Simon Maganga  baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na kesi.

Maganga alikuwa anakabiliwa na mashtaka sita likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya ShSh55.6 milioni.

Mhasibu huyo amefutiwa kesi hiyo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai  ( CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),  Maghela Ndimbo akisidiana na Nickson Shayo ameieleza mahakama hiyo leo Jumatano Julai 24, 2019 mbele ya hakimu Mkazi Mkuu,  Thomas Simba  wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya utajwa.

Ndimbo amedai DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya mshtakiwa kuomba kuiondoa mahakamani.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka, amesema analiondoa mahakamani kama upande wa mashtaka walivyoeleza.

Pia Soma

Maganga alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu Julai 11, 2018 akikabiliwa na  mashtaka hayo katika kesi ya uhujumu uchumi  namba 49/2018.

Maganga anadaiwa Januari 2009 alimdanganya mwajiri wake kwa kutumia vocha za kuwasilisha mbegu za pamba katika msimu wa mwaka  2009/10 akijaribu kuonyesha kampuni ya Afrisian Ginning Limited  ilinunua mbegu za pamba kilo 25.1milioni.

Pia, Maganga alifanya hivyo kwa kampuni ya Nyanza Cooperative Limited  kwa kuonyesha kuwa ilinunua kilo 3.7milioni za mbegu za pamba wakati akijua siyo kweli.

Katika shtaka lingine, mshtakiwa anadaiwa kutumia vocha za kuwasilisha mbegu za pamba msimu wa 2009/10 akijaribu kuonyesha Kampuni ya S&C Ginning Limited ilinunua kilo 17.1milioni za mbegu za pamba.

Maganga akiwa kama mhasibu wa TCB, alifanya ufujaji na ubadhirifu wa fedha kiasi cha Sh55.6 milioni mali ya TCB.

Chanzo: mwananchi.co.tz