Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mhasibu Udart kizimbani kwa madai ya kughushi

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Alphonce Kika (29), Mhasibu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka 36 ya kughushi tiketi za mabasi hayo.

Akisoma hati ya mashtaka leo Jumanne Aprili 30 mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde, wakili wa Serikali, Jenifa Masue amedai kuwa, mshtakiwa alitenda kosa hilo Aprili 17 mwaka huu katika kituo cha mabasi ya Udart ,Mbezi wilaya ya Ubungo.

Imedaiwa kuwa, Aprili 18 mwaka huu akiwa kituoni hapo, mshtakiwa alighushi tiketi 36 za mabasi ya kampuni hiyo akionyesha ni halali na zimetolewa na kampuni hiyo wakati akijua si kweli.

Mshitakiwa alikana mashitaka yote na upande wa mashtaka ulieleza upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Kasonde alimtaka mshitakiwa huyo kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua za utambulisho kutoka Serikali ya mtaa anaoishi atakayesaini bondi ya Sh20milioni.

Mahakama pia imemtaka mshitakiwa huyo kutotembelea vituo vya mabasi hayo ya Udart na kwenye ofisi zao.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 13 huku mshtakiwa  akirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhama.



Chanzo: mwananchi.co.tz