Arusha. Mhadhiri wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, Haliye Haliye amefikishwa mahakamani ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za kuomba rushwa kwa wanafunzi ili kuwasaidia wafaulu mitihani wa marudio.
Amefikishwa mahakamani leo Alhamisi Desemba 12, 2019 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akizungumza leo mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Frida Wikes amesema mhadhiri huyo akiwa anawafundisha wanafunzi wa astashahada aliwashawishi wampatie fedha ili awasaidie wafaulu mtihani wa marudio.
Wiles amesema uchunguzi wa Takukuru umebaini kuwa mtuhumiwa aliomba kupewa Sh50,000 kwa kila mwanafunzi.
"Alitumia ushawishi huo kupitia mwanafunzi ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu ya uchunguzi. Huyo mwanafunzi alipokea fedha kutoka kwa wanafunzi wenzake na kuzituma kwa mwalimu huyo kupitia miamala ya simu na benki,” amesema Wiles.
Amesema baada ya uchunguzi kukamilika, mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani leo kwa tuhuma za kushawishi, kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na 11/2007.
Wikes amewataka wanafunzi kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa ili elimu wanayoipata kihalali iwe na tija.