Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mhadhili Msaidizi NIT anusurika kifungo cha miaka mitatu jela, alipa faini

85903 PIC+NIT Mhadhili Msaidizi NIT anusurika kifungo cha miaka mitatu jela, alipa faini

Tue, 26 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mhadhili Msaidizi wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Samson Mahimbo (69), amehukumiwa kulipa fidia ya Sh2 milioni na faini ya Sh5 milioni au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukiri  kutumia mamlaka yake kumlazimisha mwanafunzi Victoria Faustine kutoa rushwa ya ngono.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi alisema kifungu cha 25 cha Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007 inasema mtu yeyote ambaye yupo kwenye nafasi na akatumia nafasi hiyo kuomba rushwa ya ngono kwa kigezo cha kumpa kazi, atakuwa amefanya kosa na atashtakiwa na adhabu yake ni faini ya Sh5 milioni au kwenda jela miaka mitatu.

Shaidi alisema hakuna ubishi kitendo alichofanya ni cha aibu kwa umri wake na taaluma yake anapaswa kuwa mtu mzuri lakini mshtakiwa akaamua kujiingiza katika mapenzi na watoto wadogo.

Alisema vitendo vya rushwa ya ngono imekuwa gumzo kwa vyuo vingi nchini, hivyo inapaswa kupingwa, kuonyesha majibu kwa watoto ni kuwaua kitaaluma na matokeo yake tunapata wataalamu waliofaulu isiyo njia sahihi.

“Watu kama wewe wanatakiwa waletwe mahakamani ili wapatiwe adhabu ambayo itawafanya wajutie kitendo walichofanya, hivyo mahakama hii inakuhukumu ulipe fidia ya Sh2 milioni na faini ya Sh5 milioni ukishindwa kulipa utakwenda miaka mitatu jela,” alisema Hakimu Shaidi.

Kabla ya kutolewa kwa Hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Zakaria Ndaskoi aliiambia Mahakama hiyo kuwa hana  kumbukumbu za makosa ya nyuma za mshtakiwa, hivyo ni mkosaji wa mara ya kwanza.

Ndaskoi alisema kufuatia makubaliano ya mshtakiwa aliyoingia na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hawapendekezi kutoa adhabu kubwa hivyo mshtakiwa alikubali kulipa Sh2 milioni na ameshalipa.

Kwa upande wa utetezi, Claudio Msando aliomba isiwape adhabu nyingine kwa kuwa mshtakiwa ni mzee na anaumwa magonjwa ya uzeeni na kutoona vizuri. Pia anategemewa na familia.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa akiwa mwajiriwa wa NIT, alikuwa akifundisha wanafunzi wa muhula wa kwanza wa masomo wa mwaka  2015/16 anadaiwa kuomba rushwa hiyo kutoka kwa mwanafunzi, Victoria Faustine.

Na alitenda kosa hilo Januari 12, mwaka 2017 katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Camp David , iliyopo Mlalakuwa Mwenge.

Inadaiwa mshtakiwa huyo akiwa mwajiriwa wa NIT katika kozi ya Usimamizi wa Barabara na Usafirishaji namba LTU 07101 kwa kutumia mamlaka yake, alimlazimisha mwanafunzi huyo kutoa rushwa ya ngono.

Ilidaiwa kuwa aliomba rushwa hiyo ili aweze kumfaulisha katika mtihani  wake wa marudio katika kozi ya Usimamizi wa Barabara na Usafirishaji uliokuwa unafanyika Januari 5 , mwaka 2017.

Chanzo: mwananchi.co.tz