Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgombea ubunge aliyemuua msaidizi wa mpinzani wake atorokea Uganda

Mbunge Wa Kenya Mgombea ubunge aliyemuua msaidizi wa mpinzani wake atorokea Uganda

Thu, 11 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi nchini Kenya wamesema wanaamini kuwa Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alitorokea Uganda baada ya madai ya kumuua kwa kumpiga risasi msaidizi wa mpinzani wake.

Polisi wanaoshughulikia tukio hilo lililotokea juzi Agosti 9, 2022 wakati wa uchaguzi walisema mbunge huyo hajasalimisha kama alivyoagizwa.

Barasa, ambaye anatetea kiti chake kwa tikiti ya UDA, ameshinda ubunge tayari licha ya kutokomea kusikojulikana mpaka sasa.

Kisa hicho kilihusisha Barasa na mpinzani wake wa kisiasa Brian Khaemba wa DAP katika kituo cha kupigia kura cha Chebukwabi ambapo walipaswa kushuhudia kuhesabiwa kwa kura.

Afisa wa Upelelezi wa Jinai katika Kaunti ya Bungoma, Joseph Ondoro alisema mkasa ulitokea wakati ugomvi ulipozuka kati ya wawili hao na kumfanya Khaemba kuondoka na kuelekea kwenye gari lake.

“Barasa alimfuata akiwa na watu wanne na kuwaamuru wasimruhusu (Khaemba) kuondoka mahali hapo. Hata hivyo, dereva wa Khaemba, Joshua Nasokho alikaidi agizo hilo na kuwasha gari hilo,” Ondoro alisema.

Hapo ndipo Barasa anaripotiwa kuchomoa bastola na kumfyatulia. Alipata majeraha makubwa yaliyosababisha kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kimilili.

Ondoro alisema wanamtafuta Barasa kuhusu tukio hilo. “Amekimbia lakini tunamtafuta. Ajisalimishe,” alisema na kuongeza kuwa wameanzisha msako wa kuwasaka watu wake wa karibu lakini bado wanasaka maeneo yote ambayo Barasa huenda amejificha na amezima simu yake.

“Tunashuku alichukua pikipiki kuelekea Uganda lakini tutampata. Bado hajakamatwa,” alisema Ondoro na kuongeza kwamba eneo ambalo kisa hicho kilitokea ni karibu na mpaka wa Kenya na Uganda ambapo kikosi kimetumwa eneo hilo kumtafuta mbunge huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live