Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mganga mkuu akana wajawazito kutozwa 150,000/-

02704d270beb34dc9cfe68d3aeb61f83.jpeg Mganga mkuu akana wajawazito kutozwa 150,000/-

Thu, 20 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MGANGA Mkuu wa Hospital Teule ya Mkoa wa Songwe Vwawa, Lukombodzo Lulandala, amewataka wajawazito kuhudhuria na wanaojifungulia katika vituo vya afya na hospitali ya rufaa ya mkoa kwa kuwa huduma za kujifungua hutolewa bure.

Aliyasema hayo kutokana na kuwepo taarifa zilizodai kuwa, hospital hiyo ya mkoa imekuwa ikiwatoza fedha akina mama wajawazito na wanaofika hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua kwa njia ya kawaida au upasuaji.

Dk Lulandala aliwaeleza waandishi wa habari hospitalini hapo kuwa, baadhi ya taarifa zimekuwa zikisambaa kuwa hospitali hiyo ya mkoa hutoza wajawazito fedha pindi wanapojifungua.

Alisema akina mama wanaojifungua kwa upasuaji na wale wote wanaojifungua kawaida kwa mujibu wa mwongozo, huhudumiwa bure wanapokwenda kujifungulia katika hospitali ya rufaa.

"Hospitali yetu ya Mkoa wa Songwe (Vwawa) inatoa huduma za uzazi kwa kufuata Mwongozo na Sera ya Afya, kwa mama yeyote mjamzito wakati wa kujifungua huduma hutolewa bure ama iwe anajifungua kwa kawaida, au kwa upusuaji kuanzia kitanda, huduma ya mtalaamu awe daktari, au muuguzi hutolewa bure bila kutozwa kiasi chochote," alisema Dk Lulandala.

Akaongeza:"Kuna baadhi ya watu wanasambaza taarifa ambazo si za kweli kuwa akina mama wanapojifungua kwa njia ya kawaida hutozwa Sh 150,000 na anayejifungua kwa upasuaji hutozwa Sh 200,000 katika hospitali yetu ya rufa.|

“Naomba taarifa hizi zipuuzwe, lakini pia natoa mwito kwa watumishi wote kuwa wasiwatoze akina mama wanapojifungua."

Dk Lulandala alisema katika sera ya afya, pia kuna kipengele cha uchangiaji huduma ambazo ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa, ambazo muda mwingine huwa ni changamoto kupatikana , hivyo huwashirikisha wananchi ili waweze kuchangia.

Kwa upande wao akina mama waliojifungulia katika Hospitali Teule ya Mkoa wa Songwe, walisema wanafurahishwa na huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo kwa kuwa wanapewa huduma zote bure.

Mmoja wa akina mama waliojifungua kwa njia ya upasuaji, Enjoy Kalinga, alisema tangu afike hospitalini hapo licha ya kujifungua kwa upasuaji, hajachangia kiasi chochote huku akiwa amepata ushirikiano mkubwa kwa madaktari na wauguzi.

"Nina siku nne toka nijifungue kwa oparesheni, naendelea vizuri mpaka sasa na wala sijachangia kiasi chochote, madaktari wamenihudumia vizuri mpaka sasa,” alisema Enjoy.

Naye Joyce Ngaya kutoka Kijiji cha Mbimba wilayani Mbozi, alisema alipata ushirikiano wakati wa kujifungua na hakutozwa fedha.

Chanzo: www.habarileo.co.tz