Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfanyabiashara wa madini aliyedaiwa kutekwa apatikana

40776 Pic+madini Mfanyabiashara wa madini aliyedaiwa kutekwa apatikana

Mon, 11 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfanyabiashara wa madini aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha amepatikana jijini Dar es Salaam na kusimulia kilichomkuta.

Jeremiah Kituyo, ambaye ni mkazi wa Sekei Arusha, alisema mchana wa Januari 28 alikwenda eneo wanakouza majeneza jirani na chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mount Meru na akiwa hapo, watu ambao hajawatambua mpaka sasa walikamata kwa nguvu na kumuingiza kwenye gari.

“Ilikuwa ni tukio la ghafla, watu wanne wakanivamia na kuniingiza kwenye gari aina ya Landcruiser LX nyeupe na kufungwa kitambaa, safari ikaanza sikufahamu wananipeleka wapi.

“Tulisafiri kwa muda mrefu hadi kufika Dar, nilipelekwa kwenye nyumba lakini muda wote nilikuwa nimefungwa kitambaa hivyo sikuweza kujua niko wapi,” alisimulia alipozungumza na mwandishi wetu kwa simu.

Kituyo ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha madalali wa madini Mkoa wa Arusha, alieleza kuwa akiwa huko watu hao walikuwa wakimpiga na kumhoji mambo mbalimbali ambayo hakutaka kuyaweka wazi lakini yalikuwa yakihusu biashara.

Alisema watu hao waliendelea kumshikilia kwa siku nane mfululizo wakimhamisha kwenye nyumba tatu tofauti hadi Jumanne iliyopita, saa tatu usiku walipomtupa katika eneo la wazi Msasani.

Katika kipindi hicho, Kitui alidai kuwa alikuwa akipigwa na alipata majeraha kwenye mikono yake yote miwili pamoja na mbavu na kwamba aliachwa na maumivu makali kichwani.

“Walivyonitupa pale baada ya muda mfupi watu wakaniona na kuanza kunihoji nikawaelezea kwa kifupi nikiwa na maumivu na kuwatajia mawasiliano ya mdogo wangu ambaye alifika eneo la tukio wakanichukua na kunipeleka kituo cha polisi Oysterbay,”

“Nikiwa njiani nilipoteza fahamu lakini taarifa nilizopewa nilipelekwa polisi wakatupa RB kisha wakanipeleka Hospitali ya TMJ kwa ajili ya matibabu ila hali yangu haikuwa nzuri wakanipa rufaa ya kwenda Muhimbili,” alisema.

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, John Stephen alisema Jeremiah alipokewa hospitalini hapo na kupatiwa matibabu ya awali kisha kuruhusiwa.

“Alipokewa Februari 5 Saa 9:40 usiku akapatiwa matibabu na kisha kuwekwa mapumziko hadi Februari 6 Saa 10 jioni aliporuhusiwa kurejea nyumbani,” alisema Stephen.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mussa Taibu alisema hajapata taarifa kuhusu tukio hilo.

“Halijafika mezani kwangu hivyo silifahamu ila niwakumbushe wananchi kuwa neno kutekwa lisichukuliwe kirahisi ni ishu kubwa, lisiwe linatumika katika mazingira ambayo hayana uhusiano na neno lenyewe,” alisema Kamanda Taibu.

Janeth, ambaye ni mke wa Jeremiah akizungumza na Mwananchi alisema amepitia kipindi kigumu yeye na watoto wake katika kipindi ambacho mumewe alikuwa hajulikani alipo.

Alisema hakuweza kuwasiliana na mumewe tangu alipotekwa hadi Jumanne iliyopita saa nne asubuhi alipompigia simu na kumjulisha kuwa yupo salama.

Aliwashukuru waumini wenzake na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Sekei, Arusha ambao walikuwa wanawatunza kipindi cha matatizo hayo.

Alisema siku ya tukio, walikuwa kwenye msiba wa mtoto wa jirani yao

“Tulihangaika sana, lakini sikupata majibu nikabaki katika sintofahamu hadi hiyo siku ya msiba wa mtoto wa jirani yetu aliponipigia simu kuwa yuko salama,” alisema Janeth.



Chanzo: mwananchi.co.tz