Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfanyabiashara maarufu kortini akidaiwa kuua mlinzi

6d7eadd2191437c3d41fa9249d4a8722 Mfanyabiashara maarufu kortini akidaiwa kuua mlinzi

Wed, 25 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MFANYABIASHARA maarufu jijini Arusha, Lazarus Mafie (60) maarufu kwa jina la Shidolya, anayemiliki kampuni za usafirishaji watalii, hoteli na nyumba za kulala wageni, amepandishwa kizimbani kujibu shitaka la mauaji.

Shidolya alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha kujibu mashitaka mauaji ya kukusudia ya mfanyakazi wake wa nyumbani kwa kutumia kitu kinachodaiwa kuwa na ncha kali.

Shidolya ambaye ni mkazi wa Kata ya Kimandolu jijini hapa, anatuhumiwa kutenda kosa hilo akiwa na wenzake wawili wanadaiwa kumuua Furanael Mbise aliyekuwa mlinzi nyumbani kwake.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kwa kumkata na kitu kinachodaiwa kuwa chenye ncha kali na kisha kudanganya ndugu wa marehemu, jirani na marafiki kuwa mlinzi huyo ameuawa na majambazi.

Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Gwanta Mwankuga, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Naomi Mollel alidai mshtakiwa huyo na wenzake wawili walitenda kosa hilo Oktoba 18, mwaka huu nyumbani kwa mfanyabiashara huyo maarufu.

Mollel aliwataja washitakiwa wengine kuwa ni Joseph Mafie (45), mkazi wa Usa River na Joachim Mwanakatwe 26) au Baraka ambaye ni mtunza bustani wa Kampuni ya Shidolya na mkazi wa Kimandolu wilayani Arumeru.

Washitakiwa hao kwa pamoja hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na shauri hilo namba 22/2020 kuwa la mauaji na hivyo mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

Washitakiwa hao baada ya kusomewa shitaka, walipelekwa mahabusu katika Gereza Kuu la Arusha lililopo Kisongo, Arumeru kutokana na shauri hilo kutokuwa na dhamana hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Desemba 2, mwaka huu.

Mwili wa Mbise uliokuwa umehifadhiwa chumba cha maiti cha Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru umezikwa nyumbani kwake huku Shidolya akisimamia mazishi hayo ikiwamo kununua jeneza kabla ya kukamatwa na polisi akituhumiwa kuhusika na kifo cha ndugu yake huyo ambaye alimwajiri kwa shughuli za ulinzi nyumbani kwake.

Chanzo: habarileo.co.tz