Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfanyabiashara anaswa na mbolea ya ‘dili’ Kilimanjaro

Mbolea Mfanyabiashara anaswa na mbolea ya ‘dili’ Kilimanjaro

Sun, 30 Apr 2023 Chanzo: Mwananchi

Watu watatu akiwemo mfanyabiashara mmoja wa Mjini Moshi, wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, kwa kosa la kuingiza nchini Mbolea kutoka nchini jirani bila kufuata taratibu za kisheria.

Watu hao ambao walikamatwa Aprili 25, 2023 saa 5:00 usiku katika Kata ya Rau, mjini Moshi, walikutwa na mbolea zaidi ya mifuko 194 yenye ujazo wa kilo 50 kila mmoja, ambapo 141 ilikutwa kwenye gari ikisafirishwa kupelekwa sokoni huku mingine ikiwa kwenye nyumba ya mfanyabiashara huyo ambapo ilikuwa bado haijakamilika kufungashwa. Watu hao walikamatwa baada ya gari walilokuwa wakisafirishia mbolea hiyo, kukwama kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha, ambapo wananchi walilitilia mashaka na kutoa taarifa kwa viongozi wa mitaa na walipofika ndipo walikuta mbolea hiyo.

Akizungumza jana Jumamosi, Aprili 29, 2023, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kukamatwa kwa watu hao ambapo amesema mbolea hiyo iliingizwa nchini na mfanyabiashara mmoja mkazi wa Moshi na Bomang'ombe Wilaya ya Hai, ambaye jina lake wanalihifadhi. Kamanda amesema watu hao walikamatwa wakiwa na gari aina ya fuso likiwa limebeba mbolea mifuko 141 yenye ujazo wa kilo 50 kwa kila mfuko, kutoka nchi jirani. Aidha amesema baada ya kukamata mbolea hiyo, walifanya upekuzi katika nyumba ya mfanyabiashara huyo na kukuta mifuko mingine 36 ya mbolea aina ya Urea borabora na 17 ya mbolea aina ya Yara na yote ikiwa na ujazo wa kilo 50 kwa kila mifuko. “Katika upekuzi huo pia ilikutwa mifuko mitupu 691 ya mbolea aina ya Denald, mifuko 635 ya mbolea aina ya Organic Minjingu, mifuko 635 ya mbolea aina ya MPK, mifuko 117 ya mbolea aina ya Yara, mifuko 173 ya mbolea aina ya CAN, Mifuko 126 ya mbolea aina ya borabora na mifuko 141 ya mbolea aina ya DAP,”amesema. Ameongeza kuwa “Pia ilikutwa mifuko 18 ya mbolea aina ya CAS PLUS, mifuko mitupu 178 ya mbegu za mahindi Hybrid kutoka nchi jirani, pamoja na madumu madogo manne,” amesema. Kamanda amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mfanyabiashara huyo, amekuwa na tabia ya kuingiza mbolea kutoka nchi jirani bila kufuata utaratibu wa vibali na huwenda inachakachuliwa kabla ya kuingizwa sokoni. “Tunaendelea kuwashikilia watuhumiwa wote watatu kwa upelelezi wa kina, huku tukishirikiana na idara nyingine zenye mamlaka ya kisheria kuhusu utaratibu wa uingizaji wa bidhaa ya kilimo nchini na baada ya uchunguzi huo, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani,” amesema. Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori amesema mfanyabiashara aliyekamatwa anauza pembejeo za kilimo katika eneo la Mbuyuni mjini Moshi na kwamba sehemu ya mbolea iliyokutwa kwenye nyumba ilikuwa bado haijafungashwa kwenye mifuko. “Mbolea zaidi ya mifuko 140 ilikutwa kwenye gari lakini katika nyumba ya mfanyabiashara huyo ambayo haiishi familia, kulikutwa na mbolea ambayo haijafungashwa kwenye mifuko na kuna mifuko ya mbolea aina mbalimbali na mbegu ambayo ni mitupu, mmiliki wa mali hizo ambaye ni mfanyabiashara na watu wengine wawili wanashikiliwa,” amesema “Vyombo vya Dola vinaendelea una uchunguzi wa tukio hili, kwani hata kwenye upekuzi kuna vitu pia vimekutwa ambavyo haviko kwenye utaratibu wa biashara halali, hivyo baada ya uchunguzi, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika,”amesema. Diwani wa Kata ya Rau, William Kiwia amesema wana wasiwasi kuwa mbolea hiyo iliyokamatwa ipo ya Ruzuku ambayo imetolewa na Serikali kwa sababu katika eneo hilo mbolea hiyo ilikuwa ikifungashwa kwa upya kwenye mifuko na kwenda kuuzwa sokoni. “Nilipigiwa simu na wananchi na nilipofika niliona kunahitajika vyombo vya usalama, ambapo nilitoa taarifa polisi na walipofika tulipoingia katika nyumba ambayo inadaiwa kuchakachua mbolea ya ruzuku na kuweka kwenye mifuko mingine, tulikuta mbolea nyingi ikiendelea kufungashwa kwenye mifuko ya Urea, ikiwemo inayotoka nchi jirani,” amesema. Kwa upande wake jirani wa eneo hilo, Elvis Ngowi amesema kwa kipindi chote wamekuwa wakifahamu kuwa mfanyabiashara huyo anatengeneza matenga ya nyanya na hawakuwahi kufahamu kama kuna kazi ya kufungasha mbolea inafanyika eneo hilo. “Siku zote sisi tunaona mafuso yanaingia na kutoka, likiingua tunafikiri limeinguza mbao na likitoka tunajua limebeba matenga ya nyanya, lakini leo tuneshangaa baada ya kukwama, tumeona ni mbolea, kwakweli hatukuwahi kujua kama kuna mbolea inafungashwa pale, tukio hili ni baya tuombe serikali iwe makini na kuwa macho kufuatilia vitu kama hivi,” ameeleza.

Chanzo: Mwananchi