Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfanyabiashara ahukumiwa kwa kosa la kutoa rushwa

Cff795c5c5dabfc66deede36d994a3da Mfanyabiashara ahukumiwa kwa kosa la kutoa rushwa

Sun, 4 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu mfanyabiashara, Muhammad Hyderi, kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini ya Sh 500,000 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutoa rushwa.

Hyderi alikuhumiwa kifungo hicho jana na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya aliyesema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka dhidi ya mshitakiwa.

Hakimu Isaya alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi wanane waliothibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa na kuwa mbali na adhabu hiyo, pia imetaifisha Sh 2,000,000 alizotoa mshitakiwa huyo kwa ajili ya kumpa rushwa ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Mahakamaha imeridhishwa na ushahidi wa upande wa mashitaka hivyo inakuhukumu kulipa faini ya Sh 500,000 au kwenda jela miaka mitatu,” alisema Hakimu Isaya.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Nickson Shayo, aliiomba mahakama itaifishe fedha kiasi cha Sh 2,000,000 ambazo mshitakiwa alizihusisha katika kutoa rushwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 15, 2019 katika mgahawa wa Best Bites uliopo katika Wilaya ya Kinondoni baada ya kutoa rushwa ya Sh 2,000, 000 kwa ofisa wa TRA, Talib Komba ili apunguziwe kodi.

Chanzo: habarileo.co.tz