Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfanyabiashara Peter Zakaria apata dhamana

48762 Zakaripic

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Mfanyabiashara maarufu mikoa ya Kanda ya Ziwa, Peter Zakaria aliyekuwa akisota mahabusu tangu Julai 5, 2018 ameachiwa kwa dhamana.

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga amethibitisha Zakaria kuachiwa kwa dhamana tangu Machi 25, 2019.

“Hajafutiwa kesi. Bali kaachiwa kwa dhamana,” amesema DPP alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Machi 26, 2019

Hata hivyo, DPP Mganga aliyesema yuko kwenye kikao hakufafanua zaidi sababu na mazingira ya mfanyabiashara huyo kuachiwa kwa dhamana.

Zakaria alitiwa mbaroni na polisi Juni 29, 2018 kabla ya kufikishwa mahakamani Julai 5, 2018 kwa shtaka la kujaribu kuwaua kwa kuwapiga risasi Ahmed Segule na Isaac Bwire.

Ingawa hati ya mashtaka haikutaja kazi wa wawili hao wanaodaiwa kutaka kuuawa na Zakaria, mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima aliwaambia waandishi wa habari kuwa walikuwa maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Licha ya kupata dhamana Julai 10, 2018 katika kesi ya jaribio la kuua, Zakaria ambaye pia ni kada wa CCM aliendelea kusota rumande baada ya kukosa dhamana katika kesi ya uhujumu uchumi. Pia anadaiwa kumiliki bunduki aina ya shotgun na risasi tano kinyume cha sheria.

Kesi zote mbili za mfanyabiashara huyo anayetetewa na Mawakili Kassim Gila na Onyango Otieno zinatajwa mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Musoma, Rahimu Mushi ambaye ameiambia Mwananchi kuwa mashauri hayo yatatajwa kesho Machi 27, 2019.

Kuanzia saa 12:00 jioni ya Machi 25, taarifa za mfanyabiashara huyo kuonekana mitaani zilianza kuzagaaa lakini si Mahakama wala ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Musoma iliyokuwa tayari kuzungumzia suala hilo.

Ingawa watu wa karibu wa mfanyabiashara huyo anayemiliki kampuni ya Mabasi ya Zakaria yanayosafiri kati ya mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza waliithibitishia Mwananchi kumuona akiwa pamoja na baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki ndani ya gari lenye rangi jeupe wakitokea mjini Musoma kwenda nyumbani kwake mjini Tarime.

Mwanasheria wa Serikali anayesimamia kesi zake, Valence Mayenga, hakuwa tayari kuzungumza lolote akisema si msemaji huku Hakimu Mushi akieleza kuwa anachojua ni kwamba shauri hilo litatajwa Machi 27, 2019.

Utata kuhusu suala la Zakaria uliongezwa zaidi baada ya walinzi wa Mahakama kuwazuia waandishi wa habari waliofika eneo hilo wakidai muda wa mahakama ulikuwa umeisha licha ya ukweli kwamba wakati huo kundi la watu, wakiwemo baadhi ya wafanyabiashara na ndugu wa Zakaria walikuwepo kwenye ya viunga vya mahakama.

Soma Zaidi>>>Upelelezi kesi ya Mfanyabishara Zakaria haujakamilika

Soma Zaidi>>>Zakaria anyimwa dhamana, ‘apelekwa’ Mahakama Kuu



Chanzo: mwananchi.co.tz