Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu watu wanne, kutumikia kifungo cha miaka 20 kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh32.5 milioni.
Pia, Mahakama hiyo imeamuru kutaifishwa kwa gari lilotumika kubeba vipande sita vya meno ya tembo.
Washitakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 31/ 2016 ni Solomon Mtenya, Siasa Athumani, Musa Ligagabile na Omary Sabo.
Pia Soma
- UCHOKOZI WA EDO: Hili la korosho, kuna umuhimu wa kuchutama yaishe
- Shahidi aeleza bosi wake alivyoongozana na gari lenye shehena ya dhahabu
- Mbunge ataka mashine za uvuvi zinazoshikiliwa ziachiliwe
Akisoma hukumu hiyo, Kasonde alisema katika shtaka la kwanza la kujihusisha na genge la uhalifu, washtakiwa watatumikia kifungo cha miaka mitano jela bila faini.
“Katika shitaka la pili ambalo ni kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo, washtakiwa wote kwa pamoja watatumikia kifungo cha miaka miwili jela kila mmoja bila faini,” amesema Hakimu Kasonde.
Hakimu Kasonde alisema katika shtaka la tatu, ambalo ni kukutwa na vipande sita vya meno ya tembo ndani ya gari, washtakiwa wote watatumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja.
Alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi 11 ambao walithibitisha mashtaka pasina shaka.
“Kutokana na kitendo walichofanya washtakiwa hawa, mahakama hii inawahukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hii na kwamba, adhabu hiyo inakwenda kwa pamoja.
“Pia, gari aina ya Toyota Funcargo iliyotumika kubeba meno hayo ya tembo imetaifishwa na Serikali na haki ya kukata rufaa iko wazi kwa mtu ambaye hajaridhika na hukumu hii,” amesema hakimu huyo.
Awali, kabla ya kutolewa kwa hukumu, Wakili wa Serikali, Salimu Msemo akisaidiana na Constantine Kakula, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali dhidi washtakiwa hao ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Kwa mujibu ya hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la kukutwa na vipande vya meno ya tembo.
Na wanadaiwa kutenda makosa hayo Juni 23, 2016 eneo la Kimara.
Siku ya tukio, washtakiwa walikutwa na vipande sita vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 15,000 sawa na Sh 32,565, 000 , bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.