Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linamshikilia Dornald Njonjo (30), meneja wa maabara wa tume ya madini kwa tuhuma za kuiba madini ya dhahabu mali ya Serikali ya Tanzania yenye thamani ya Sh507 milioni.
Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Julai 11, 2019 na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa imeeleza kuwa madini hayo yenye uzito wa kilo 6.244 yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye kasiki katika ofisi za wakala wa madini Masaki, jijini Dar es Salaam
Amesema Juni 29, 2019 polisi walipata taarifa kutoka kwa ofisa madini wa mkoa wa Dar es Salaam, Ally Sadick baada ya kugundua upotevu wa madini hayo yaliyokamatwa mwaka 2017 bandarini Zanzibar yakisafirishwa kinyume cha sheria.
Baada ya kupata taarifa hizo polisi walianza uchunguzi mara moja na kubaini kuwa madini hayo yaliibiwa na Njonjo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya mtuhumiwa kuhojiwa alikiri kuiba kidogo tangu Desemba 2018 na kueleza kuwa aliyauza katika duka la kuuzia vito vya dhahabu huku akifanya mpango wa kuyarudishia kwa kuweka madini bandia.
Katika hatua nyingine jeshi hilo linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuvunja maduka na kuiba bidhaa mbalimbali pamoja na Bajaji mbili.
Pia Soma
- Benki ya UBA Tanzania yasaidia vitabu shule za Sekondari wilayani Kigamboni
- Muungano wa Tigo na Zantel utakuza uchumi nchini
- TEF waitaka Serikali ya Tanzania kutoa maelezo kuhusu Azory Gwanda
Pia jeshi hilo limekamata silaha moja aina ya bastola Fatin 13-Turkey yenye namba T.0622010J00535 ikiwa na risasi tisa.
Silaha hiyo ilikamatwa usiku wa Julai 4, 2019 eneo la Mbezi Tangibovu ambako kikosi maalum cha kuzuia na kupambana na majambazi kilimkuta nayo Michael Stellu.