Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Meneja Uwezeshaji wa Kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga reli ya kisasa (SGR), Yetkin Gen Mehmen kulipa faini ya Sh100 milioni au kwenda jela miaka mitatu huku ikitaifisha dola za Marekani 84, 850 alizoshindwa kuzitolea maelezo baada ya kukutwa nazo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA)
Mehmen ambaye ni raia wa Uturuki amehukumiwa na mahakama hiyo leo Alhamisi Februari, 27, 2020 baada ya kukiri kosa la kushindwa kutoa tamko ama maelezo ya fedha alizokutwa nazo dola za Marekani 84,850 katika Uwanja wa Ndege wa JNIA.
Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema kutokana na mshtakiwa huyo kukiri kosa lake mahakama hiyo imemtia hatiani.
"Mahakama inakuhumu kulipa faini ya Sh100 milioni au kwenda jela miaka mitatu pia fedha ulizokutwa nazo ambazo dola za Kimarekani 84,850 zinataifishwa na kuwa mali ya Serikali ya Tanzania," amesema Simba.
Awali Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro alimsomea hati ya mashtaka mshtakiwa huyo kuwa Februari 13, 2020 eneo la Uwanja wa Ndege wa JNIA, alikamatwa akiwa na begi la mkononi ndani yake kukiwa na dola za Marekani 84,850.
Kimaro alidai baada ya mshtakiwa huyo kukamatwa na dola hizo maofisa wa polisi walipomuuliza alishindwa kuzitolea maelezo.
Pia Soma
- Polisi yasema aliyeuawa Singida hakuwa kiongozi wa Chadema
- VIDEO: Mmiliki wa hoteli aeleza kilichotokea kwa mfanyabiashara wa Mwanza anayedaiwa kumpiga risasi mpenzi wake
- Upande wa mashtaka kujibu hoja za Rugemalira anayetaka Mahakama imuondolee kesi ya uhujumu uchumi