Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meneja benki ya CRDB korti akituhumiwa kuiba mamilioni

68836 Meneja+pic

Tue, 30 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Meneja wa benki ya CRDB, tawi la Tegeta, Dar es Salaam nchini Tanzania, Daudi Nyandwi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka nane likiwemo la kuisababishia hasara benki hiyo kiasi cha Sh 138 milioni.

Nyandwi maarufu kama Mcheche, amefikishwa mahakama hapo jana Jumatatu Julai 29, 2019 na kusomewa mashtaka yake, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali ya Tanzania, Sylvia Mitanto amedai katika shtaka la kwanza na la pili, mshtakiwa anadaiwa kati ya Novemba 18 na 20, 2014, katika benki ya CRDB, tawi la Tegeta, alighushi nyaraka ya mchanganuo wa malipo.

Katika shtaka la tatu, Nyandwi anadaiwa Novemba 21, 2014, alighushi vocha ya malipo akionyesha benki ilikuwa inadaiwa Sh113 milioni, wakati akijua kuwa ni uongo.

Mitanto alidai katika shtaka la nne na tano, Nyandwi anadaiwa kati ya Novemba 20 na 21, 2014, akiwa na nia ovu, aliwasilisha nyaraka hizo kwa Carington Shayo, akionyesha kuwa kiasi  cha Sh25 milioni kilikuwa kinadaiwa kama vocha ya malipo.

Katika shtaka sita, Novemba 20, 2014, Nyandwi akiwa kama meneja na mtumishi wa benki hiyo, aliiba Sh25 milioni mali ya CRDB.

Pia Soma

Vile vile, Novemba 21, 2014, katika benki hiyo, mshtakiwa akiwa mfanyakazi wa benki hiyo, aliiba Sh113 milioni mali ya benki hiyo.

Katika shtaka la nane, mshtakiwa anadaiwa Novemba 21, 2014 katika benki ya CRDB tawi la Tegeta wilaya Kinondoni, Nyandwi akiwa Meneja wa benki wa tawi hilo, aliisababishia benki hiyo hasara ya Sh138 milioni.

Mshtakiwa alikana mashtaka yanayomkabili na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shuari hilo bado haujakamilika.

Hakimu Simba alitoa masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao watasaini bondi ya Sh70 milioni  kila mmoja.

Pia mmoja wa wadhamini hao anatakiwa kuwasilisha hati ya nyumba au mali isiyohamishika mahakamani hapo.

Hata hivyo mshtakiwa huyo ameshindwa kutimiza masharti na kurudishwa rumande.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 7, 2019 itakapotaja.

Chanzo: mwananchi.co.tz