Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mdee, wenzake wafutiwa kesi ya vurugu gerezani

B033a1faa12b75c13c484d915a820c80.jpeg Mdee, wenzake wafutiwa kesi ya vurugu gerezani

Thu, 6 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewafutia kesi wabunge Halima Mdee, Esther Bulaya na wafuasi 25 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mdee na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya mkusanyiko haramu na kuvunja geti la Gereza la Segerea.

Kesi hiyo ilifutwa jana baada ya upande wa mashitaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaid alifuta kesi hiyo kwa kuzingatia kifungu cha 225(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinachompa hakimu mamlaka ya kufuta kesi ikiwa upande wa mashitaka utashindwa kupeleka mashahidi kwa muda mrefu. Kifungu hicho pia kinaruhusu Jeshi la Polisi liwakamate tena washitakiwa ikiwa upande wa mashitaka una nia ya kuwafungulia mashitaka mapya.

Awali upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mkunde Mshanga akisaidiana na Wakili wa Serikali Esther Martin ulidai kuwa kesi hiyo ilipelekwa kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi lakini waliomba tarehe nyingine kwa kuwa hawakuwa na shahidi mahakamani hapo.

Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala na Edson Kilatu ulipinga kuahirishwa kwa kesi hiyo na ukaiomba Mahakama iifute kwa kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuleta mashahidi kwa muda mrefu.

“Kesi hii imeshakuwa na maahirisho kwa muda mrefu hivyo ninawaachia washitakiwa chini ya kifungu cha 225(5)” alisema Hakimu Shaidi.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Jesca Kishoa, Boniface Jacob, Patrick Assenga, Henry Kilewo, Yohana Kaunya, Kedmony Mhembo, Mshewa Karua, Khadija Mwago na Pendo Raphael maarufu Mwasomola, Cesilia Michael, Happy Abdalla; Stephen Kitomali, Paul Makali, Edgar Adelin na Reginald Masawe. Katika kesi hiyo washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashitaka saba yakiwemo ya kutoa lugha ya kuudhi, kuharibu mali, kufanya mkusanyiko usio kuwa wa halali, kutotii amri halali iliyowekwa na Jeshi la Magereza na shambulio.

Ilidaiwa kuwa Machi 13 mwaka jana katika eneo la Gereza la Segerea, lililopo wilaya ya Ilala, kwa makusudi washitakiwa hao walikaidi amri halali ya kuondoka eneo la gereza.

Pia washitakiwa hao walidaiwa kuharibu geti kuu la kuingilia na kutokea katika Gereza la Segerea na pia Mdee, Bulaya na Jacob walidaiwa kutoa lugha ya matusi kwa askari Magereza aliyekuwa akisimamia usalama getini hapo.

Aidha mshitakiwa Jacob alidaiwa kumshambulia askari Magereza kwa kumvuta shati na kumchania wakati akiwa katika utekeleza wa majukumu ya ulinzi katika eneo hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz