Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchungaji aja na dawa ya Panya Road

Panya Road Mei Panya Road

Sat, 24 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiongozi wa Kanisa la The Word of Reconciliation Ministries, Nabii Nicholous Suguye, ametaja mbinu za kubaini vikundi vya vijana vinavyofanya vitendo vya uhalifu, maarufu kama Panya Road.

Moja ya hatua hizo, kwa mujibu wa Suguye, ni jamii kushirikiana na serikali katika kudhibiti vitendo hivyo ili nchi kuwa na amani katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa mkutano wa injili uliofanyika jijini Arusha, Nabii Suguye alisema, jamii ina nafasi kubwa ya kuisaidia serikali kukomesha vitendo vya uhalifu kutokana na vijana hao kuwa sehemu ya jamii yenyewe.

"Vitendo hivi vya uhalifu vinafanywa na vijana wadogo ambao bado wanahitaji uangalizi wa karibu wa wazazi au walezi, hivyo kwa kuunganisha nguvu kwa pamoja itasaidia kukomesha vitendo hivi" alisema.

Alisema, jambo la kusikitika ni kuona vikundi vya Panya Road vinaundwa na vijana wadogo ambao ni tegemeo kwa baadaye na kwamba kama jamii itafumbia macho,  kutakuwa na wimbi kubwa la vijana wasiokuwa na maadili katika taifa.

"Vijana hawa ni nguvu kazi inayotegemewa katika familia na taifa kwa ujumla. Tusipoamua kuisaidia serikali yetu kwa kukemea na kuwafichua, tutatengeneza kizazi kisichofaa katika taifa na kusababisha  hasara kubwa kwenye jamii,” alisema.

Kiongozi huyo alisifu kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la polisi limekuwa katika kupambana na uhalifu, hivyo wananchi wanapaswa kuliunga mkono kwa kutoa ushirikiano kuwabaini wahalifu hao ili kuendelea kuishi kwa usalama na amani.

Nabii Suguye, alitumia nafasi hiyo kufanya maombezi maalum ya kuiombea nchi na serikali sambamba na kumwombea afya njema Rais Samia Suluhu Hassan, ili aendelee kutimiza majukumu yake.

Vikundi vya Panya Road ambavyo vimekuwa vikiibuka na kutoweka mara kwa mara, mapema mwezi huu viliripotiwa kutikisa maeneo kadhaa mkoani Dar es Salaam na kupora vitu mbalimbali kama fedha, simu, kujeruhi na kuua mtu mmoja.

Kutokana na hali hiyo, serikali mkoani Dar es Salaam ilitangaza hatua za kukabili vikundi hivyo vinavyohusisha watoto wa miaka kati ya 11 na 15 ikiwamo kuwakamata na kuwachukulia hatua.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, alitangaza kuwa askari polisi 300 wameletwa mkoano humo pamoja na na magari kadhaa ya doria kwa ajili ya kupambana na uhalifu huo.

Siku moja baada ya kauli hiyo, polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam walitangaza kuwaua vijana sita wanaodaiwa kuwa Panya Road, ambao walikuwa katika kutekeleza uhalifu.

Aidha, Bunge pia liliingilia kati na kutaka serikali kuchukua hatua zinazostahili kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa haraka. Wabunge pia waliomba kuahirisha kwa muda shughuli za Bunge katika mkutano uliomalizika jana jijinio Dodoma ili kujadili suala hilo ambalo pia limeaathiri baadhi yao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live