Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchimba madini auawa Chato kwa kukatwa mapanga

PANGA Ed Mchimba madini auawa Chato kwa kukatwa mapanga

Sun, 6 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchimbaji mdogo wa dhahabu, Tegemeo Msure (38), mkazi wa kijiji cha Ihanga kilichopo kata ya Buziku, wilaya ya Chato, mkoani Geita ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na kichwani.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea Novemba 2, 2022 na kwamba kabla ya kuuawa, wauaji walitumia bunduki ya AK47 kumtisha ili asimame akiwa kwenye pikipiki yake.

Anasema baada ya kutishwa, alisimama na walimkamata wakamfunga kwa kamba ya katani shingoni na kumzungushia tumboni na mikononi na kumburuza hadi umbali wa mita 170 toka eneo aliposimamishwa na kufanikisha azma yao ya mauaji kwa kumkatakata mapanga,” amesema Jongo.

Kamanda ameeleza wakati wakitekeleza mauaji hayo alitokea msamaria mwema akitaka kumuokoa marehemu lakini wauaji walifyatua risasi hewani ili kumtisha ashindwe kutoa msaada.

Amesema kwenye eneo la tukio limeokotwa ganda la risasi moja inayotumika kwenye silaha ya AK47.

Kufuatia tukio hilo, kikosi cha kupambana na ujambazi kimefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne ambapo watatu ni Watanzania na mmoja ni raia wa Burundi anayedaiwa kuingia nchini na silaha hiyo ambayo haina usajili.

“Tulipowakamata watuhumiwa hao baada ya mahojiano walionyesha silaha aina ya AK47 ambayo haina namba za usajili ikiwa na risasi 11. Silaha hiyo ilikuwa imefichwa kwenye mpaka wa shamba la mahindi huko Buziku na wahusika wamekiri kufanya mauaji hayo,” amesema Kamanda huyo.

Kamanda Jongo amesema bado wanaendelea na upelelezi na ukikamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live