Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge CCM mbaroni tuhuma ujangili

Thu, 7 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga, linamshikilia Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi, kwa tuhuma za kukutwa na silaha na nyara za serikali nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Debora Magiligimba, mbunge huyo anadaiwa kukutwa na nyara za serikali zilitokana na uwindaji haramu kwenye eneo la Negezi wilayani Kishapu, huku gari lenye namba za usajili T 760 DSD Nissani Hardbody likidaiwa kutumika kwa shughuli hiyo.

Alisema mbunge huyo alikamatwa Mei 3 mwaka huu saa 5:45 usiku, akiwa nyumbani kwake, Mtaa wa Lubaga mjini Shinyanga.

Kamanda Magiligimba alisema kikosi kazi cha askari wa upelelezi wa makosa ya jinai wakiongozwa na David Msangi, wakiwa na ofisa wanyamapori, Perfect Mbwambo, walimkata mbunge huyo nyumbani kwake akiwa na nyara za serikali pamoja na silaha.

"Walipofanya upekuzi nyumbani kwa mbunge huyo, walifanikiwa kukamata nyama inayodhaniwa kuwa ni ya wanyamapori yenye uzito wa kilogramu 35 zikiwa zimehifadhiwa kwenye jokofu lililokuwa jikoni na nyingine sehemu ya mazoezi pamoja na kwenye gari, na katika gari hilo, ilikutwa silaha Shotgun yenye namba 46092.

"Katika chumba chake cha kulala, zilipatikana silaha zingine 15 ambazo ni Tzcar 87342, aina ya Air Gun, Tzcar 63729 Rifle, Tzcar 77325, Rifle, Tzcar 87636 Markiv, Tzcar 65673 Rifle, Tzcar 72731 Rifle.

"Tzcar 87342 Airgun, Tzcar 53933 Rifle, Airgun Cz 455 Rifle, Cz 537-2 Rifle, 978836- Mod 151 Shotgun, Pistol aina ya Browning 061738, na kufanya jumla ya silaha zilizokamatwa kuwa 16 na risasi 536 zikiwa kwenye kabati la nguo," alisema.

Magiligimba alisema baada ya uchunguzi kufanyika, waligundua silaha 10 kati ya 16 anazimiliki isivyo halali na kwamba sampuli za nyama wamezipeleka kwenye Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi.

Alisema upelelezi ukikamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili, huku akitoa onyo kwa yeyote wanaojihusisha na vitendo vya kumiliki silaha isivyo halali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live